Habari za Kitaifa

Dumisheni uaminifu mkipiga vita ufisadi, Pareno ahimiza kamati za kaunti

Na STANLEY NGOTHO December 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Katibu wa Wizara ya Haki, Haki za Binadamu na Masuala ya Katiba, Bi Judith Pareno, aliwahimiza wanachama wa Kamati za Uangalizi wa Wananchi Dhidi ya Ufisadi za Kaunti (CACCOCs),  kuhakikisha wanafanya kazi yao kwa uaminifu na uwajibikaji.

“Serikali inashirikiana na washirika wa maendeleo kutafuta mbinu shirikishi ya kukabiliana na utamaduni wa ufisadi unaokwamisha maendeleo ya nchi,” alisema Bi Pareno.

Alisema hayo Jumanne katika Chuo Kikuu cha Cooperative wakati wa uzinduzi wa warsha ya wanachama wa  kamati hizo zinazolenga kujumuisha wananchi katika vita dhidi ya ufisadi ambayo ilihudhuriwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.

Aliongeza kuwa serikali itahakikisha usalama wa wanaotoa taarifa kuhusu ufisadi ili kuzuia vitisho na unyanyasaji.

“Tutaongeza ulinzi kwa wale wanaofichua ufisadi dhidi ya mitandao ya wahusika wanaojaribu kuwatisha. Serikali inahitaji wananchi wake kushiriki katika vita hivi  hadi ngazi za mashinani,” alisema.

Bw Felix Koskei, alitoa wito kwa Wakenya kushirikiana na serikali katika vita dhidi ya ufisadi ambao kwa miaka mingi umeathiri utoaji wa huduma za serikali.

Bw Koskei amesema kwamba licha ya hatua nyingi ambazo serikali ya Rais William Ruto imeweka kukabili janga hilo, ufisadi bado umeenea katika ngazi za mashinani kote nchini.

Amesisitiza Wakenya wana uwezo mkubwa kupitia mitandao ya kijamii kurekodi na kufichua maafisa wala rushwa kwa kutumia simu zao.

“Serikali imejizatiti kung’oa ufisadi ili kuboresha huduma kwa umma. Serikali kupitia taasisi husika iko tayari kumshtaki kila mfisadi, lakini Wakenya lazima wasimame na kutumia nguvu ya mitandao ya kijamii kuwafichua wanaoendeleza ufisadi,” alisema Bw Koskei.

Uzinduzi huo uliambatana na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kukabiliana na Ufisadi iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa.

Kamati hizo kutoka kaunti zote 47 zinajumuisha wawakilishi kutoka Baraza la Makanisa (IRCK), Maendeleo ya Wanawake (MYWO), Baraza la Vijana (NYC), Baraza la Watu Wenye Ulemavu (NCPWD) na wanahabari.

Mafunzo ya siku tatu yanalenga kuwaelimisha wawakilishi wa CACCOC mbinu bora za kuendesha kampeni za uhamasisho kuhusu madhara ya ufisadi, jinsi ya kuripoti visa katika njia sahihi kisheria na kufuatilia hatua zinazochukuliwa.

Bw Koskei alisema wanatarajia wawakilishi hao kuwa mabalozi wa kupambana na ufisadi katika maeneo ya mashinani