e-Citizen: Mawaziri wanne matatani wakidaiwa kupuuza mahakama
Mawaziri wanne huenda wakajipata matatani kwa kuendelea kukusanya ada ya Sh50 kutoka kwa Wakenya wanaotumia jukwaa la malipo la e-Citizen.
Katika ombi alilowasilisha katika Mahakama Kuu, mwanaharakati Dkt Magare-Gikenyi anataka Mawaziri John Mbadi, Kipchumba Murkomen, William Kabogo na Julius Ogamba, watajwe kuwa wamedharau mahakama kwa kuendelea kukusanya ada hiyo licha ya amri ya kusitisha utozaji huo kutolewa.
Dkt Gikenyi pia anataka Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) Humphrey Wattanga na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor, waadhibiwe kwa dai la kukaidi amri ya mahakama kuhusiana na agizo hilo.
Katika uamuzi uliotolewa Aprili 1, Jaji Chacha Mwita alipiga marufuku serikali kutoza na kukusanya ada ya Sh50 ya huduma, au kiasi chochote kwa kila muamala unaofanywa kupitia jukwaa la e-Citizen kama ada ya huduma.
Dkt Gikenyi alisema mawaziri hao wanapaswa kubeba lawama binafsi kwa hasara yoyote isiyo halali na isiyo ya kikatiba inayotokana na kutozwa kwa ada hiyo anayosema ni haramu.

“Mlalamishi (Dkt Gikenyi) amegundua kuwa licha ya uamuzi wa mahakama, washtakiwa wameendelea kutoza na kukusanya ada hiyo kutoka kwa Wakenya na watumiaji wa e-Citizen kinyume cha sheria na kinyume na uamuzi wa mahakama hii tukufu,” alisema Dkt Gikenyi.
Ada hiyo ya Sh50 kwa kila muamala au dola moja kwa miamala ya fedha za kigeni, hutozwa isipokuwa Waziri wa Fedha aamue kuiondoa.Daktari huyo kutoka Nakuru alisema uamuzi huo wa mahakama ulikuwa wazi kabisa na kwamba maafisa wa serikali walipaswa kuutii.
Aidha, aliongeza kuwa utamaduni wa kukaidi maagizo ya mahakama bila kuogopa umezidi na ni lazima mahakama zitumie mamlaka yake ya kikatiba kuwaadhibu wanaokaidi.
“Uamuzi huo ulipotolewa, ulikuwa wa kutekelezwa na si wa kupuuzwa, hadi pale ambapo mahakama ya juu zaidi itautengua au mahakama hii yenyewe iubatilishe. Hakuna amri ya kusitisha utekelezaji iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa au mahakama nyingine yoyote yenye mamlaka, wala uamuzi huo haujafutwa,” alisema.

Katika uamuzi wake, Jaji Mwita alisema ada ya Sh50 ilikuwa sawa na kutoza mara mbili kwa huduma moja, na kwamba wananchi hawawezi kulazimishwa kutumia mfumo ambao hawakuutaka na kisha kubebeshwa jukumu la kuufadhili kwa kulipa ada ya ziada.
Pia, jaji huyo alifutilia mbali agizo la serikali lililotaka karo za shule na ada nyingine zilipwe kupitia jukwaa la e-Citizen.
“Hili ni jambo lisilo na mantiki na lisilokubalika. Hakukuwa na maelezo yoyote kuhusu ni nani anayepokea ada hiyo ya huduma na inatumiwa kufanya nini, jambo linalofanya ada hiyo kuwa haramu,” alisema jaji.
Amri hiyo pia iliwazuia mawaziri wa Fedha, ICT na Uchumi wa Kidijitali, pamoja na Waziri wa Elimu na wawakilishi wao, kutaka karo za shule zilipwe kupitia e-Citizen.