E-Citizen pigo kwa wazazi wanaolipa karo kupitia kwa bidhaa za shambani
MFUMO mpya wa kulipa karo kidijitali kupitia tovuti ya e-Citizen umezua kizungumkuti kwa wazazi wanaotegemea mbinu mbadala kuwezesha watoto wao kupata elimu.
Katika shule nyingi za mashinani, wazazi huafikiana na usimamizi wa taasisi za elimu kuhusu mbinu mbadala za kulipa karo ikiwemo mazao ya kilimo, kuchanja kuni au kuteka maji.
Hata hivyo, mpango wa kulipa karo kidijitali ulioanzishwa na serikali ya Rais William Ruto kama njia ya kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za shule, sasa unatishia kukatiza elimu ya watoto kutoka familia maskini.
Mabadiliko hayo yamezua suitafahamu kwa baadhi ya wazazi nchini.
Bw Mbuya Okado, mkazi wa Mbita, Kaunti ya Homabay, ana maafikiano maalum na shule mbili yanayowezesha wanawe kuendelea kupata elimu.
Baada ya kuvuna, Bw Okado ambaye ni mkulima katika Kijiji cha Ngodhe, hupeleka sehemu ya mazao yake ya sukumawiki na mahindi katika shule za sekondari eneo hilo, yanayotumika kwenye mpango wa lishe shuleni.
“Kwa sababu watoto wangu wanasomea katika shule mbili ambapo mimi hupeleka mazao, pesa ninazostahili kulipwa hutumika kuwalipia karo,” anasema Bw Okado.
Mkulima huyo anasema amekuwa akitumia mpangilio huo wa malipo kuelimisha watoto wake watatu akiwemo mmoja aliyefanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka uliopita.
Katika juhudi za kuangamiza ufisadi, serikali imepanga kubadilisha huduma zote za umma ili zitolewe kidijitali.
Kulingana na Rais Ruto, matumizi ya e-Citizen ni njia ya kuhakikisha kuwa walimu wakuu wa shule hawaanzishi ada haramu, hivyo kuwazidishia wazazi mzigo wa karo.
Mahakama Kuu jijini Nairobi ilisitisha kwa muda matumizi ya tovuti hiyo ikielezea hofu kuwa matumizi yake kulipa karo huenda yakazuia watoto maskini kupata elimu.
Mbunge wa Ndhiwa Martin Owino ameitaka serikali kufutilia mbali mfumo huo akisema ingawa baadhi ya wazazi wanaweza kulipa karo kwa urahisi kidijitali, kunao wasioweza kuutumia hivyo basi watoto wao huenda wakafukuzwa shuleni kwa kutolipa karo.
Hii inajumuisha wazazi wanaotumia mbinu mbadala na mikataba maalum kuelimisha watoto wao.
“Baadhi ya wazazi ambao ni wakulima wanaweza kukubaliana na shule wawe wakipeleka mazao ya kilimo kama karo. Hii haiwezi ikatekelezwa kupitia e-Citizen,” alisema.
Bw Owino alisema changamoto za kifedha zinazoandama familia nyingi zitasababisha baadhi ya watoto kukosa elimu.
“Baadhi ya wazazi wamelemewa na changamoto za kifedha kiasi kuwa wanaweza tu kulipa karo kupitia mbinu mbadala ambapo wanapeleka mboga, kuni, nafaka na bidhaa nyinginezo zinazogeuzwa karo ya watoto wao,” alisema.
Mbunge huyo alisema hayo katika hafla ambapo aligawa Sh23 milioni za basari kwa watoto maskini katika shule za sekondari.
Huku akiitaka serikali kubatilisha uamuzi wa kulipa karo kupitia e-citizen, mbunge huyo alisema kuwa kuwashurutisha wazazi kufanya hivyo kutahujumu azma ya kuendeleza usawa wa elimu kwa watoto wote Wakenya.