Habari za Kitaifa

E-Citizen yaigeuza Kenya mnara wa Babeli

February 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

HATUA ya Baraza la Mawaziri mnamo Jumatano kuidhinisha ulipaji karo katika taasisi zote za elimu kupitia mtandao wa e-Citizen, imeongeza migawanyiko ambayo imekuwepo nchini kuhusu pendekezo hilo.

Hatua hiyo ilifuatia kikao cha baraza hilo, kilichoongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Hilo lilijiri siku moja tu, baada ya Mahakama Kuu kuongeza muda wa agizo linaloizuia serikali kuzilazimisha shule na taasisi nyingine za elimu kukumbatia mfumo huo kwenye ulipaji karo na ada zile nyingine.

Wadau katika sekta ya elimu wameeleza wasiwasi wao kuhusu ukumbatiaji wa matumizi ya mfumo huo kuhusu ulipaji karo.

Licha ya serikali kusisitiza kuwa mtandao huo ni salama, baadhi ya wadau wamejitokeza na kueleza hofu yao kwamba huenda ukaanza kukumbwa na matatizo, kama vile kuchelewa kwa fedha zinazopaswa kuzifikia taasisi tofauti.

Baadhi ya wadau ambao wamejitokeza kueleza hofu zao ni Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Sekondari na Vyuo Anuwai (Kuppet) Akelo Misori, aliyesema kuwa chama hicho kitawaongoza walimu wakuu wa shule za upili kupinga agizo hilo la serikali.

“Tumepokea malalamishi mengi kutoka kwa walimu wakuu kwamba, bado hawajapewa maelezo ya kutosha kuhusu vile watakuwa wakifikiwa na pesa zinazolipwa kama karo. Je, pesa hizo zitakuwa zikiiendea wizara na baadaye serikali kuwatumia? Ni baada ya muda upi ambao watakuwa wakitumiwa pesa hizo? Kuna kiwango kitakachotolewa kutoka kwa karo hiyo? Hayo ni baadhi tu ya maswali ambayo tungeitaka wizara kutufafanulia,” akasema Misori.

Katibu Mkuu wa Kuppet Bw Akelo Misori ahutubia wanahabari mnamo Jumanne, Januari 10, 2023, kuangazia masaibu ya watahini wa karatasi za majibu ya watahiniwa wa mtihani wa KCSE. PICHA | DENNIS ONSONGO

Kulingana na Bw Christopher Mutai, ambaye mwanawe ni mwanafunzi katika mojawapo ya shule za upili za kitaifa nchini, mfumo huo utazua matatizo mengi kwa wazazi ambao wamekuwa wakikubaliana na walimu wakuu kuhusu njia na utaratibu watakaozingatia kwenye ulipaji wa karo hiyo.

“Kuna wazazi ambao wamekuwa wakikumbwa na matatizo mengi kwenye ulipaji karo. Baadhi yao wamekuwa wakilipa karo kwa kuwasilisha bidhaa kama mahindi, maharagwe au hata mchele. Huo huwa ni mpango wanaokubaliana na walimu wakuu wa shule husika. Mfumo huo utawaathiri sana,” akasema Bw Mutai.

Bw Martin Ndirangu, ambaye ni mtaalamu na msimamizi wa mfumo wa IFMISS katika mojawapo ya kaunti hapa nchini, alisema kuwa lazima serikali ihakikishe kuwa fedha zinazolipwa kwa taasisi fulani kupitia mtandao wa e-Citizen zimezifikia kwa wakati ufaao.

“Kuna changamoto nyingi za kimitambo ambazo zimekuwa zikijitokeza kwenye mfumo wa malipo kupitia mitandao. Hilo ndilo limekuwa likichangia ucheleweshaji wa pesa zinazotumwa kwa kaunti tofauti kupitia mfumo wa IFMIS,” akasema Bw Ndirangu.

Hata hivyo, serikali imetetea vikali mfumo huo, ikisema utahakikisha uwazi na uwajibikaji kuhusu pesa zinazolipiwa huduma zake.

Kulingana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Wilson Sossion, mfumo huo ndio njia ya pekee serikali inaweza kuhakikisha kuna uwazi kwenye matumizi ya pesa zinazolipiwa huduma zake.

“Kwenye ulipaji karo ya shule, hii ni njia nzuri sana, kwani itahakikisha kuwa kuna uwajibikaji kwenye matumizi ya pes azote zinazolipwa kwa shule husika,” akasema Bw Sossion.

Katibu wa Idara ya Uhamiaji Julius Bitok anashikilia kwamba serikali imeweka mikakati ya kutosha kuepuka changamoto zozote za kimitambo ambazo huenda zikatokea.

Katibu wa Idara ya Uhamiaji Julius Bitok ahutubia wanahabari baada ya kufanya kikao na makatibu wa wizara, maafisa wakuu watendaji na wenyeviti wa bodi za mashirika 17 ya serikali kuangazia namna ya kuhakikisha malipo ya huduma kwa eCitizen na nambari moja maalum ya paybill yanafanikishwa. PICHA | WILFRED NYANGARESI