EACC, ODPP na Muturi wapinga mswada wa marekebisho ya sheria kupambana na ufisadi
NA CHARLES WASONGA
ASASI za serikali zinazohusika katika vita dhidi ya ufisadi zimepinga mswada wa marekebisho ya sheria za ufisadi zinazozuia uovu huo katika mchakato wa ununuzi wa bidhaa.
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, Afisi ya Mwanasheria Mkuu na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) zinasema Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi ya 2023 uliodhaminiwa na Mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku unahujumu vita dhidi ya ufisadi.
Mswada huo, ambao unashughulikiwa na Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC), unapendekeza kuondolewa kwa sehemu za 45 (2) b na c za sheria ya awali zinazoharamisha kutozingatiwa kwa sheria za ununuzi wa umma.
Aidha, mswada huo unatoa nafasi kwa utekelezaji wa miradi kabla ya mipango kufanywa.
Kwenye memoranda yake kwa JLAC inayoongozwa na Mbunge wa Tharaka George Murugara, EACC inashikilia kuwa kuondolewa kwa makosa hayo mawili ya ufisadi kutatoa mwanya wa watu wafisadi kuendela kupora nchi hii.
“Ununuzi wa umma unachangia kati ya asilimia 10 na 13 ya Jumla ya Utajiri wa Kitaifa na hivyo pesa za umma zinazotumika katika ununuzi huo zinapasa kulindwa,” EACC ikasema.
Kwa upande wake afisi ya Mwanasheria Mkuu Justin Muturi ilisema kuwa marekebisho yaliyopendekezwa yanaenda kinyume na “sera ya kupambana na ufisadi na mikataba ya kimataifa inayohitaji kuboreshwa kwa sheria kupambana na ufisadi.”
“Ni sawa kwa mswada huo kuondoa makosa na ukiukaji wa sheria katika ununuzi wa bidhaa za umma katika orodha ya vitendo vya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi,” ikasema taarifa kutoka kwa afisi ya Bw Muturi.
ODPP ilisema kuwa pendekezo la kufutiliwa mbali kwa sehemu ya 45 (2) b litasababisha athari kubwa kwa mwongozo wa kisheria wa kulinda wizi wa pesa za umma.
“Michako ya ununuzi wa bidhaa hukumbwa na hatari ya ufisadi haswa katika utumishi wa umma. Hivyo, ipo haja kuhakikisha kuwa sheria za sasa ununuzi unazingatiwa ili kukinga mali ya umma wakati wa ununuzi katika utumishi wa umma,” afisi hiyo ikasema.
ODPP inashikilia kuwa kuwepo kwa kosa na kutekeleza mradi bila mipango ya mapema kulilenga kukinga serikali kutokana na hatari ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Shirika la kupambana na ufisadi, Transparency International (TI) pia limepinga mswada huo.
“Mswada huo unaenda kinyume na masilahi ya umma, kanuni za usimamizi wa pesa za umma, viwango vya uongozi na utawala bora na uwajibikaji,” akasema mkurugenzi Mkuu wa TI Sheila Masinde.