Habari za Kitaifa

EACC yakomboa ‘jumba la jaji’ miongoni mwa mali za wizi

May 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

TITUS OMINDE Na LABAAN SHABAAN

MAKAZI ya jaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Eldoret ni miongoni mwa mali za umma za thamani ya Sh3.2 bilioni ambazo zimekuwa mikononi mwa wanyakuzi.

Lakini Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imefaulu kutwaa mali hizi zilizoporwa na wezi wenye ushawishi mkubwa katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Nyingi ya mali zilizotwaliwa zinahusishwa na kampuni za watu na familia za tabaka la juu pamoja na viongozi wenye ushawishi mkubwa waliokuwa katika serikali ya chama cha uhuru cha KANU – baadhi yao wameaga dunia.

Wakati uo huo, EACC imefichua kuwa Chuo Kikuu cha Moi ni mojawapo ya taasisi za umma ambazo ni kitovu cha visa vya ufisadi.

Kulingana na tume hiyo, mali zilizonyakuliwa Eldoret ni za mahakama, polisi wa utawala, Hospitali ya Rufaa ya Uasin Gishu, kituo cha kuzima moto cha kaunti na Bunge la Kaunti.

Ajabu ‘jumba la jaji’ kuwa miongoni mwa mali za wizi zilizokombolewa na EACC. PICHA | MAKTABA

Nyumba nyingi za serikali zilizoibiwa ziko katika mtaa wa kifahari wa Elgon View.

Haya ni kwa mujibu wa msemaji wa EACC Eric Ngumbi.

Bw Ngumbi alifichua ardhi hiyo ilinyakuliwa na kampuni za kibinafsi zinazomilikiwa na watu mashuhuri, kwa ushirikiano na maafisa wa ardhi wafisadi.

EACC inaarifu hati miliki za ardhi iliyotwaliwa awali zilikuwa mikononi mwa watu wenye utajiri mkubwa.

Mali nyingine 97 zenye thamani ya Sh7.4 bilioni mjini Eldoret bado zinadaiwa kumilikiwa na makateli lakini uchunguzi unaendelea.

“Tumetwaa ardhi ya umma yenye thamani ya Sh3.2 bilioni. Ardhi ambayo tumeipata, ilinyakuliwa na kampuni za kibinafsi zinazomilikiwa na watu mashuhuri,” Bw Ngumbi alisema katika warsha ya kuangazia ufisadi iliyohusisha mabunge ya kaunti za Vihiga, Elgeyo Marakwet, na Kisumu.

Mkurugenzi wa EACC Kanda ya North Rift Charles Rasugu alisema visa vya unyakuzi wa ardhi ya umma vinaongezeka katika eneo hilo.

“Unyakuzi wa ardhi umekithiri na tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha ardhi inarudishwa kupanua eneo la ustawishaji kabla Eldoret haijakuwa jiji rasmi,” alisema Bw Rasugu.

Wakati uo huo, tume hiyo imedokeza kuwa inashirikiana na Chuo Kikuu cha Moi kusaidia kubaini mianya ya ufisadi katika chuo hicho.

Baadhi ya vyuo vikuu vinatuhumiwa kwa kuchangia ongezeko la vyeti ghushi.

“Vyuo vikuu vingine vinatoa vyeti ghushi ili kupata pesa na kushusha viwango vyetu vya elimu,” alisema Bw Ngumbi.

Haya yanajiri wakati wafanyakazi zaidi ya 10 wa Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia vyeti ghushi vya masomo ili kupata ajira.