• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
EACC yaondolea Chiloba kesi ya ufisadi iliyopelekea kutimuliwa Tume ya Mawasiliano

EACC yaondolea Chiloba kesi ya ufisadi iliyopelekea kutimuliwa Tume ya Mawasiliano

EDNA MWENDA NA FATUMA BARIKI

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imetamatisha upelelezi dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Mawasiliano nchini (CAK) kuhusu madai ya ubadhirifu wa pesa.

Kupitia taarifa iliyoandikiwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa mamlaka hiyo David Mugonyi, Tume hiyo imesema uchunguzi wao ulioanzishwa Septemba 2023 haukupata ushahidi wa kutosha kuendeleza kesi.

“Uchunguzi wetu umebaini kwamba hakuna ushahidi wa kutosha kuendeleza mashtaka dhidi ya Ezra Chiloba na maafisa wengine wa Tume ya Mawasiliano kuhusu ununuzi wa nyumba,” ikasema barua hiyo iliyoandikwa Aprili 4, 2024 na kutolewa Alhamisi.

Bw Chiloba alisimamishwa kazi katikati ya Septemba kufuatia madai ya matumizi mabaya ya mamlaka na kutofuata sheria.

Alijiuzulu wadhifa huo mwezi mmoja baadaye.

Mkuu wa Upelelezi wa EACC Pascal Mweu alikuwa ameitisha stakabadhi kutoka kwa tume hiyo ili kusaidia katika uchunguzi.

Barua hiyo ilimtaka Kaimu Mkurugenzi Mkuu Christopher Wambua apeane ripoti za ukaguzi kutoka Wizara ya Fedha, mpango wa ununuzi wa nyumba wa tume hiyo, madaftari ya mikopo na orodha ya wakadiriaji thamani ili kusaidia katika uchunguzi.

Kulingana na EACC, wakadiriaji thamani walitaja kiasi cha pesa ambacho hakikuwiana na ukadiriaji uliofanywa na serikali na jambo hilo likaleta tashwishi.

Bw Chiloba alidaiwa kutofuata sheria ambako kulitokana na madai ya yeye mwenyewe kujiidhinishia ununuzi wa nyumba ambao ulipaishwa thamani mara zaidi ya thuluthi tatu na yeye pia kuwa muuzaji na mnunuzi wa nyumba hiyo.

Maswali yaliibuliwa wakati ilibainika kwamba Tume ilituma pesa kwa akaunti ya kibinafsi ya Chiloba ambaye alijiweka kama mnunuzi.

Kuondolewa kwa kesi kunajiri wakati Chiloba anafanyiwa mahojiano kwa ajili ya wadhifa wa Ubalozi jijini Los Angeles, Amerika alioteuliwa na Rais William Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Vibanda vyachomwa mzozo kuhusu mji wa Keroka ukichacha

Israel yaua wana 3 wa kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh

T L