EACC yaonya kuhusu ongezeko la wapelelezi feki wanaotapeli watu pesa
TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeonya kuhusu ongezeko la watu wanaodai kuwa wapelelezi wake huku wakitapeli watu pesa.
Kulingana na EACC, idadi ya watu waliokamatwa wakijifanya wapelelezi wake nchini imeongezeka hadi zaidi ya 300 kufikia Agosti 2024.
EACC sasa inaonya kuwa walaghai wanaojifanya wapelelezi wa tume hiyo wanawalenga Wakenya wasio na habari ili kuwatapeli pesa zao walizochuma kwa bidii.
Mwaka huu pekee, EACC imeelezea kupokea visa zaidi ya 300 vya watu wanaojifanya maafisa wa tume hiyo au wa mashirika mengine ya kutekeleza sheria
Msemaji wa EACC, Bw Eric Ngumbi, alifichua kuwa baadhi ya visa hivyo vimeripotiwa kaunti za Kakamega, Bungoma na Busia, ambako walaghai wameanzisha afisi feki za EACC na kudai wanatoa huduma za EACC.
Kwa mfano, huko Busia, inadaiwa kuwa taasisi kwa jina Shirika la Uchunguzi wa Kupambana na Ufisadi limekuwa likipokea pesa kutoka kwa umma kushughulikia mizozo inayohusiana na ufisadi.
EACC imeshangazwa na jinsi Wakenya wengi wako tayari kutoa hongo ili wawawe kujinusuru dhidi ya madai wanayohusishwa nayo.
Wapelelezi wengine bandia hufanya uchunguzi, kukamata watu, na kufanya upekuzi na kisha kudai hongo wakiahidi kuondoa mashtaka dhidi ya watu wanaowalenga.
Wengine huvamia maeneo ya biashara ya watu wakidai kuwa wanakagua uzingatiaji wa mahitaji mbalimbali ya leseni au kusaka bidhaa ghushi.
“Walaghai hao wamekuwa wakiwalenga maafisa wa serikali katika serikali ya kitaifa, maafisa wa kaunti, wakuu wa shule na maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa na wafanyabiashara wa kibinafsi, huku wengi wao wakipoteza mamilioni ya pesa,” EACC imefichua.
Kwa wakuu wa shule, walaghai hao huzingatia madai ya malipo haramu ya ada, ununuzi na masuala ya usimamizi wa fedha.
Katika kaunti hizo, walaghai hao hulenga maafisa wanaofanya kazi katika ukusanyaji wa mapato huku kwa maafisa wa utawala wa Serikali ya Kitaifa, wakiwahusisha na madai ya ufisadi.
Bw Ngumbi asema Wakenya wanaokumbana na watu wanaotiliwa shaka wanapaswa kuarifu EACC ili kuepuka walaghai.
“Umma unahimizwa kuwasiliana na EACC na kuthibitisha ukweli kuhusu watu wanaodai kuwa maafisa wake,” amesema Bw Ngumbi.
Mwezi uliopita, EACC ilimkamata afisa wa polisi anayehudumu katika Kituo cha Polisi cha Muthangari na watu wengine wanne walipovamia nyumba ya afisa wa Kaunti ya Kitui wakijifanya makachero wa tume hiyo.