Echesa alazwa Karen huku vijana wakitisha kuandamana
RICHARD MUNGUTI Na SHABAN MAKOKHA
POLISI wamempeleka aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa katika hospitali ya Karen kutibiwa, baada ya hali yake ya afya kudorora katika kituo cha polisi cha Muthaiga alikozuiliwa tangu Alhamisi jioni.
Mawakili Danstan Omari na Cliff Ombeta walithibitishia Taifa Leo kwamba Bw Echesa aliondolewa kutoka kituo cha polisi cha Muthaiga na kupelekwa Karen Hospital mnamo Jumamosi anakoendelea kupokea matibabu.
Na wakati huo huo, mmoja wa viongozi wa vijana katika eneo la Mumias ametisha kuandaa maandamano, kushinikiza kuachiliwa kwa Bw Echesa.
Anadai kuwa Bw Echesa anadhulumiwa na serikali ya Kenya Kwanza aliyoifanyia kampeni kushinda wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.
Bw Abdalla Mushefa alisema vijana watafanya maandamano makubwa kuishurutisha idara ya polisi kumwachilia Bw Echesa.
“Endapo Bw Echesa hatakuwa ameachiliwa ifikapo Jumapili, tutaelezea ulimwengu ujumbe mkali,” Bw Mushefa alieleza wanahabari mjini Mumias.
Kiongozi huyo wa vijana alisema polisi hawana haki kumnyima mshukiwa dhamana ikiwa ni mgonjwa.
“Tunataka kujua sababu ya kukamatwa kwa ndugu yetu na sababu ya kumnyima dhamana. Polisi hawapaswi kutumiwa kusuluhisha tofauti za kisiasa,” alisema Bw Mushefa.
Mnamo Ijumaa, mawakili Omari na Ombeta pamoja na Seneta wa Kakamega Dkt Boni Khalwale, walifika katika makao makuu ya Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) kuomba Bw Echesa aachiliwe kwa dhamana, ama apelekwe hospitalini wakidai ni mgonjwa.
Bw Echesa aliyekamatwa Alhamisi, alizuiliwa katika kituo cha Polisi cha Muthaiga na hatimaye kupelekwa DCI kuhojiwa kwa madai ya kujiteka nyara na kudai pesa kwa vitisho.
Polisi walisema wanamhoji Bw Echesa kutokana na madai ya kutoa vitisho kwa Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa. Inadaiwa alimtisha gavana huyo na kumtaka atoe pesa ili video chafu aliyorekodiwa isisambazwe katika mitandao ya kijamii.
Baada ya kukamatwa, mshukiwa huyo aliye pia mwenyekiti wa Shirika la Kenya Water Towers Agency, alieleza polisi ni mgonjwa na kwamba anahitaji matibabu ya dharura baada ya kufanyiwa upasuaji.
“Mteja wetu anahitaji matibabu ya dharura. Polisi wamekataa kumwachilia na hali yake imezidi kudorora,” Bw Omari akawaambia wanahabari katika makao makuu ya DCI Ijumaa alasiri.
Lakini Jumamosi polisi walimpeleka Karen Hospital kupokea matibabu.
Bw Echesa anatarijiwa kufikishwa kortini Aprili 2, 2024.
Mnamo Februari 2024 Mahakama kuu iliamuru Bw Echesa ashtakiwe kwa kashfa ya uuzaji wa silaha za thamani ya Sh39.5 bilioni.
Huku haya yakijiri vijana walioelezea wasi wasi wao kuhusu hali ya Bw Echesa walielezea hofu yao kuhusu hali ya waziri huyo wa zamani.
Bw Echesa alikamatwa kufuatia madai ya mwanasiasa kutoka kakamega kwamba alidai pesa kutoka kwake (mwanasiasa) kwa vitisho.
Bw Echesa aliagizwa afike DCI kuhojiwa kisha akakamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga.
Vijana hao wamedai kuna watu wanaomfitini Bw Echesa na kutoa wito kwa Rais William Ruto aingilie kati na kuzima dhuluma dhidi ya mwenyekiti huyo wa shirika la uhifadhi wa maji.