Habari za Kitaifa

Endeleeni kuwekeza nyumbani, Wetang’ula ahimiza Wakenya walio ng’ambo

Na  BENSON MATHEKA January 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amepongeza juhudi na bidii ya Wakenya wanaoishi  na kufanya kazi ng’ambo kwa kujitahidi kuimarisha maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii.

Akizungumza pembezoni mwa mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CSPOC) uliofanyika  visiwa vya Guernsey, Visiwa vya Channel, alipokutana na Wakenya wanaoishi humo, Bw  Wetang’ula aliwapongeza kwa uvumilivu wao katika maisha ya ughaibuni huku wakiendelea kudumisha urithi wao wa kiafrika..

“Inatia moyo kuona Guernsey, yenye idadi ya watu takribani 65,000, ikiwa mwenyeji wa jamii yenye nguvu ya Wakenya zaidi ya 500,” alisema Spika Wetang’ula. “Jamii hii imejumuika kikamilifu katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikichangia sekta muhimu kama fedha, ukarimu, na elimu.”

Bw  Wetang’ula, ambaye yuko Guernsey kwa ziara rasmi ya siku mbili, alieleza kuridhishwa kwake na juhudi za Wakenya walio ng’ambo  katika kuinua jina la Kenya kimataifa huku wakiwekeza nyumbani.

“Michango yenu inalingana na mkakati wa Serikali ya Kenya wa ajira za ughaibuni na ushirikiano, unaolenga kutumia uwezo wa Wakenya waishio nje ya nchi kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa,” alibainisha.

Akitafakari kuhusu kipindi chake kama Waziri wa Mambo ya Nje, Mheshimiwa Wetang’ula alikumbuka hatua muhimu alizochukua katika kuingiza masuala ya  raia nje ya nchi kwenye sera za mambo ya nje za Kenya.

“Nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, nilipa kipaumbele suala hili kama nguzo muhimu ya sera zetu za nje. Niliwatambua Wakenya waishio nje kama mabalozi wa nia njema wanaoitangaza na kuwakilisha Kenya ulimwenguni huku wakibaki Wakenya halisi,” alieleza.

Balozi wa Kenya nchini Uingereza, Bi Catherine Karemu, alihakikishia jamii hiyo kuwa ofisi yake iko tayari kusaidia Wakenya wa Guernsey kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa ipasavyo.

“Tumejitolea kutafuta suluhu endelevu kwa changamoto mnazokumbana nazo. Ofisi yangu itaendelea kuwezesha maisha bora na yenye utulivu kwa Wakenya hapa Guernsey,” alisema Bi Karemu.