• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
ETA: Kenya yakaangwa kuanza kuwatoza ada ‘majirani’ kuingia nchini

ETA: Kenya yakaangwa kuanza kuwatoza ada ‘majirani’ kuingia nchini

NA WANDERI KAMAU

KENYA imekosolewa vikali kwa kuanza kuwatoza ada raia kutoka mataifa ambayo hayakuwa yakihitaji viza ili raia wake kuruhusiwa kuingia nchini.

Licha ya serikali kuondoa hitaji la raia wanaoingia nchini kuwa na viza, imetangaza ada ya Sh4,500 kwa raia hao, isipokuwa wale wanaotoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hayo yanatekelezwa kupitia Mfumo wa Idhini ya Kielektroniki ya Kusafiri (ETA) kuanzia mwezi huu.

Baadhi ya mataifa ambayo yamelalamikia hatua hiyo ni Zambia na Malawi, yaliyokuwa miongoni mwa mataifa 51, ambayo raia wake hawakuwa wakihitaji viza ili kuingia nchini.

Kupitia mtandao wa X, Jumatatu, afisi ya Msemaji wa Serikali ya Malawi ilisema hatua hiyo inakinzana na nia ya kubuni “Afrika Moja.”

“Lazima tuhahikishe kuwa sera na hatua tunazoweka si kikwazo kwa juhudi za kuliunganisha bara Afrika kuwa jumuiya moja ya kisiasa na kiuchumi,” ikaeleza afisi hiyo.

Zambia, kwa upande wake, ilisema “itatoa mwelekeo kuhusu hatua hiyo”.

“Si vizuri Waafrika kuwa kikwazo cha utangamano wa raia wake kwa kuweka vizingiti visivyofaa,” ikasema Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya taifa hilo.

Shtuma hizo zinajiri huku raia wa kigeni 9,787 wa kigeni wakiwa tayari washatuma maombi ya kusafiri humu nchini bila kutumia viza, kulingana na taarifa iliyotolewa na Idara ya Uhamiaji.

Katibu wa idara hiyo, Prof Julius Bitok, alisema kuwa tayari, stakabadhi za watu 4,046 zishaidhinishwa, hivyo wako huru kuzuru nchini.

Katibu wa idara ya uhamiaji, Prof Julius Bitok akihutubu awali. PICHA | MAKTABA

Alisema kuwa stakabadhi za watu waliobaki zinafanyiwa utathmini.

Serikali ilisema uzinduzi wa mfumo huo unalenga kuharakisha mchakato wa kutathmini maombi yanayotumwa na raia.

Pia, unalenga kuimarisha usalama nchini, kwa kuhakikisha raia hao si tishio kwa usalama wa kitaifa.

Kabla ya uzinduzi wa mfumo huo, raia kutoka mataifa 51 walikuwa huru kuingia nchini bila hitaji la viza, huku raia kutoka mataifa 155 wakihitajika kulipa ada ya Sh7,500 ili kupata visa ya kuwaruhusu kuingia nchini.

Serkali ilisema ada hiyo mpya ya Sh4,500 ni kuhakikisha kuna usawa miongoni mwa raia wote wanaoingia nchini kutoka ng’ambo.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa Mukuyu walia eneo la biashara kugeuzwa dampo

KCSE: Alinur Mohamed akemewa kudai E nyingi ni sababu ya...

T L