Eti muite rais kumhoji? Mnaota, Murkomen aambia wabunge
Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, amejiunga na mjadala mkali kuhusu ikiwa Rais William Ruto anafaa kufika bungeni kutoa ushahidi kufuatia madai yake kwamba kuna ufisadi mkubwa katika Bunge.
Wabunge kwa hasira wametaka Rais aitwe bungeni kutoa ushahidi wa madai hayo ya mienendo isiyofaa.
Hata hivyo, Bw Murkomen amepuuza madai hayo akisema Rais anaweza tu kutoa ushahidi kwa taasisi za uchunguzi, na si kwa Bunge.
Awali, Bw Murkomen alijivuta kuzungumzia suala hilo, lakini aliposhinikizwa, alizungumza kwa uangalifu, akisema anatarajia pingamizi kutokana na mtazamo wake.
‘Hebu nijitose kwenye mjadala huu ingawa najua hatari zake kutokana na ghadhabu ya umma. Mimi binafsi naamini kwamba aliyosema Rais hayakulenga mtu binafsi, bali alizungumzia taasisi. Rais amewahi kutukemea kama mawaziri na hata kuwalaumu baadhi yetu hadharani kwa madai ya wizi au mambo mengine. Nilijua hakunilenga kwa sababu najijua, kwa hivyo haikuwa na maana mimi kulalamika. Wale wanaolalamikia matamshi ya Rais wanapaswa kujichunguza na kujirekebisha badala ya kumshambulia,’ alisema.
Waziri huyo, aliyekuwa akizungumza na wanahabari katika mahojiano ya kina usiku wa Alhamisi katika Kaunti ya Nyeri, alimtetea Rais akisema kwamba akiwa kiongozi wa nchi ana taarifa muhimu za kijasusi kuhusu kinachoendelea nchini, lakini taarifa hizo haziwezi kutumika kama ushahidi mahakamani. Alisema Rais alizungumza kwa nia ya kuwaonya wabunge wanaojihusisha na vitendo vya ufisadi.
Alishangaa kwa nini baadhi ya wabunge wana hofu ilhali Rais hakumtaja mtu yeyote.
Bw Murkomen, ambaye pia ni wakili, alisema wanaotaka Rais aitwe kutoa ushahidi hawana ufahamu sahihi wa sheria kwa sababu ni taasisi za uchunguzi kama Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) pekee zilizo na mamlaka hayo. Alisema iwapo Rais atataka kutoa ushahidi, basi anaweza kufanya hivyo kupitia taasisi hizo.
‘Rais hawezi kugeuza taarifa za kijasusi kuwa ushahidi unaoweza kutumika mahakamani. Kwa hivyo, kinachofanyika ni kwamba akiwa na taarifa hizo kama Rais, huzitumia kuwaonya wanaojihusisha na tabia hizo,’ alisema.
Baadhi ya wabunge wametaka Rais Ruto aitwe kutoa ushahidi kuhusu madai ya ufisadi aliyoyatoa hadharani.
Wamesisitiza kwamba yeyote anayehusishwa na madai hayo afikishwe awajibike, wakionya kuwa kutokuchukua hatua kunaweza kuharibu imani ya wananchi kwa Bunge.
Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula pamoja na Spika wa Seneti Amason Kingi, wote wamepuuzilia mbali madai ya Rais kuhusu hongo Bungeni, wakisema hakuna malalamishi rasmi yaliyowasilishwa dhidi ya wahusika.