Faida za Kenya kuwa mshirika mkuu wa Amerika asiye mwanachama wa NATO
AGGREY MUTAMBO Na CHARLES WASONGA
HATUA ya Amerika kuipa Kenya hadhi ya kuwa Mshirika wake Mkuu asiyekuwa mwanachama wa Kundi la Kujihami la Nato ni ishara ya imani kwa jeshi la taifa hili.
Lakini hatua hiyo haipandishi uhusiano huo hadi kuwa wa mkataba rasmi wa kijeshi.
Hii ina maana kuwa japo Amerika itakuwa ikiisaidia Kenya kijeshi, Amerika haitajukumika kuingilia kati kuisaidia Kenya ikishambuliwa na taifa la kigeni.
Nchi wanachama wa kundi la Nato (North Atlantic Treaty Organisation) zina wajibu kisheria kusaidiana miongoni mwao kijeshi dhidi ya adui.
Kundi la kujihami la Nato ndilo kongwe zaidi duniani.
Kwa hivyo, kulingana na Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika, Mshirika Mkuu asiye Mwanachama wa Nato (MNNA) hupata manufaa yafuatayo:
- Hukopeshwa vifaa mbalimbali vya kivita.
- Hutumika na Amerika kama kituo cha kuhifadhi silaha zake za kivita, kando na kwenye kambi za kijeshi za Amerika.
- Taifa kama hilo linaweza kushirikiana na Amerika katika nyanja ya utoaji mafunzo ya kijeshi.
- Kampuni za mshirika kama huyo (MNNA) zinaruhusiwa na mataifa wanachama wa Nato kutuma maombi ya zabuni ya kukarabati vifaa vya kijeshi vya Amerika nje ya nchi hiyo.
- Taifa kama hilo linaruhusiwa kupata ufadhili kuhusu ununuzi wa vifaa vya kugundua vilipuzi na vifaa vingine vya kupambana na ugaidi.
Tayari Amerika iko na kambi ya kijeshi katika eneo la Manda katika Kaunti ya Lamu, Pwani ya Kenya, inayotumika katika vita vyake dhidi ya ugaidi katika kanda hii.