Familia ya diwani aliyetekwa nyara yashtaki Masengeli na Amin
FAMILIA ya diwani wa Bunge la Kaunti ya Wajir Yusuf Hussein Ahmed, aliyedaiwa kutekwa nyara Ijumaa Septemba 13, 2024 jijini Nairobi, imeshtaki mkuu wa polisi nchini, ikitaka afikishwe mahakamani haraka iwezekanavyo.
Kupitia kakake Abdikadir Abdullahi Ahmed, familia hiyo inaomba Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) kumwasilisha MCA huyo wa Wadi ya Della ambaye pia ni kiongozi wa wachache katika bunge la kaunti.
Bw Ahmed, akiandamana na madiwani 35, wakiongozwa na spika Abdilleh Yusuf, walisema wana wasiwasi kwani hawajui kilichompata mwenzao tangu Septemba 13, 2024.
Katika kesi yao iliyowasilishwa na wakili Danstan Omari, familia na bunge zima la kaunti wanaitaka mahakama kumshurutisha Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli na mkuu wa DCI Mohammed Amin kuhakikisha kuwa MCA yuko salama popote alipo.
Kuhusu kisa hicho, familia hiyo inasema kuwa MCA huyo alikodi teksi iliyokuwa ikiendeshwa na Wambua Kioko kutoka Halai Estate kwenye barabara ya Muhoho, South C.
Alitakiwa kumsafirisha hadi Pangani Estate.
Bw Kioko alisema aliendesha gari kutoka Halai Estate kuelekea Mombasa Road na katika mzunguko wa barabara ya Enterprise, gari jeupe aina ya Prado ilijaribu kumpita mara mbili kisha ikapunguza mwendo.
“Ghafla Prado hiyo ambayo ilionekana kuwa katika mawasiliano na nyingine nyeupe ilinipita na kuzuia teksi niliyokuwa nikiendesha,” Kioko alisema.
Alisema watu watano walitoka kwenye gari hilo nyeusi aina ya Prado wakiwa na bunduki na kulikaribia gari lake, wakafungua milango kabla ya kumuamuru Yusuf kutoka nje.
Dereva huyo wa teksi alisema mmoja wa watekaji nyara alimlenga bunduki usoni na kumwamuru kusalimisha kila kitu alichokuwa nacho.
Alidai walichukua simu yake ya rununu, chaja, na stakabadhi kabla ya kurudi kwenye Prado nyeusi na kuondoka kwa kasi kuelekea Barabara ya Lusaka na kumuacha akiwa amekwama.
Baadaye alienda katika Kituo cha Polisi cha Eneo la Viwanda ambako aliripoti tukio hilo.
Familia hiyo ilisema tangu Ijumaa, kwa kushirikiana na madiwani 35 kutoka Kaunti ya Wajir, wametembelea vituo vyote vya polisi jijini Nairobi na hawajamuona.
Familia hiyo sasa inaitaka Mahakama Kuu iamuru IG na DCI wamwasilishe mshukiwa ndani ya saa 24.