Habari za Kitaifa

Familia ya Gen Z aliyeuawa yashtaki polisi

Na SAM KIPLAGAT August 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

FAMILIA ya kijana mwenye umri wa miaka 22 aliyeuawa mwezi Juni wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024, imeishtaki serikali.

Familia hii imechukua mwelekeo huu baada ya serikali kukosa kuwachukulia hatua maafisa wa polisi wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo.

Bi Beatrice Muthoni Kamau, dadake Beasley Kogi, alisema katika kesi hiyo iliyoidhinishwa kuwa ya dharura na Mahakama Kuu kwamba hakujakuwa na uchunguzi wowote kuhusu mauaji hayo yaliyotokea Juni 25 jijini Nairobi.

Jaji Bahati Mwamuye alimwagiza wakili wa Bi Muthoni, Dudley Ochiel kukabidhi Inspekta Jenerali wa Polisi, Mwanasheria Mkuu na Tume ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi stakabadhi za kesi kufikia Agosti 23.

Jaji Mwamuye aliagiza kesi hiyo itajwe Septemba 18, ili kuthibitisha kama wahusika watakuwa wametimiza maagizo hayo.

Bi Muthoni alisema mauaji ya kiholela ya Beasley yalikiuka haki yake ya kulindwa kwa mujibu wa Kifungu 27 cha katiba.

Alisema kukosa kwa Tume ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya maafisa wa polisi ni ukiukaji wa sheria.

‘Ibara ya 244(a) na 246(3) ya katiba inahitaji washtakiwa kuwaadhibu na kuwafungulia mashtaka maafisa wa polisi waliomuua Beasley Kogi,’ alisema kwenye hati ya kiapo.