Habari za Kitaifa

Familia ya waziri wa zamani yapoteza ardhi kwa kutoitumia kwa miaka mingi

Na  BENSON WAMBUGU August 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Familia ya aliyekuwa waziri mwenye ushawishi mkubwa katika serikali ya Rais Daniel arap Moi, marehemu Joseph Kamotho, imepoteza shamba la ekari 25 lililoko katikati ya mji wa Thika, Kaunti ya Kiambu, baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi kuamua kuwa lilimilikiwa kihalali na familia iliyoishi ndani kwa muda mrefu.

Bi Serah Wambui Kibiku alifaulu kudai umiliki wa shamba hilo, akieleza kuwa, licha ya kuuzwa kwa watu wengine tangu miaka ya 1990, familia ya Kamotho au wanunuzi hawakuwahi kuchukua umiliki wa ardhi hiyo. Mahakama ilikubaliana naye kuwa familia yake imekuwa ikiishi na kutumia ardhi hiyo tangu mwaka 1965 bila kupingwa, hivyo kupewa haki ya kumiliki.

Jaji Grace Kemei aliamuru msajili wa ardhi kufuta hatimiliki zote zilizotokana na kugawanywa kwa ardhi hiyo awali na kumtambua Bi Kibiku kama mmiliki halali wa ardhi hiyo ya thamani kubwa.

Jaji alisema kuwa waliodai kuwa walinunua kihalali hawakuonyesha kuwa walifanya uchunguzi wa kina kabla ya kununua ardhi hiyo. “Kama wangetafuta habari za umiliki, wangegundua kuwa Bi Kibiku alikuwa na haki ya umiliki tangu 2003,” alisema jaji.

Mahakama ilibaini kuwa, licha ya wanunuzi zaidi ya 30 na mwanawe Kamotho, Bi Nyokabi Kamotho, kuwa na hati miliki, hakuna ushahidi kuwa walichukua hatua yoyote kuondoa familia ya Kibiku kutoka ardhi hiyo.

Bi Kibiku alieleza kuwa mumewe, marehemu Gibson Kibiku, alipewa ruhusa ya kuishi kwenye ardhi hiyo na serikali mwaka 1965, na familia yao imekuwa ikiendesha shughuli za ufugaji, uchimbaji wa mawe, na hata kuwazika wapendwa wao humo. Ardhi hiyo inapakana na majengo ya zamani ya Castle Breweries kando ya Barabara Kuu ya Thika.

Mnamo 1987, Kamishna wa Ardhi alithibitisha kwa barua kuwa Kibiku anaweza kuendelea kutumia ardhi hiyo hadi taarifa nyingine itakapotolewa. Bi Kibiku alidai kuwa alikuwa akilipa kodi ya ardhi na kutimiza mahitaji mengine ya kisheria.

Hata hivyo, mwaka 1991, ardhi hiyo iligawa na ekari 25 kutolewa kwa kampuni ya Deacons Enterprises, inayohusishwa na Kamotho, huku ekari 5 zikitolewa kwa Bw Wambugu Nderitu. Baadaye, Bw Nderitu alishtaki familia ya Kibiku akitaka watimuliwe lakini kesi hiyo ilitupiliwa mbali mwaka 2011, na familia hiyo ikaendelea kumiliki ekari hizo 5.

Kuhusu ekari 25, licha ya kuwa na hati miliki, Kamotho au wanunuzi hawakuchukua umiliki wala kuendeleza ardhi hiyo. Kibiku alisema kuwa Kamotho alikuwa akitembelea eneo hilo mara kwa mara, hali iliyowafanya wakae ndani kwa hofu, lakini hakuwahi kuwaondoa.

Bi Nyokabi Kamotho, ambaye ni msimamizi wa mali ya baba yake, alieleza kuwa ardhi hiyo iliuzwa kwa bei ya Sh2.1 milioni na baadaye kugawanywa katika ploti ambazo zilinunuliwa na watu mbalimbali kati ya mwaka 1996 na 2002.

Mashahidi waliowakilisha wanunuzi walithibitisha kuwa walinunua ploti hizo kutoka kwa Deacons Enterprises lakini walikiri kuwa hawakufanya uchunguzi wa umiliki kabla ya kununua.

Mmoja wao, Bi Jane Wambui Mungai, alikiri kununua ploti mnamo Novemba 2008 lakini hakufanya uchunguzi wowote wa umiliki. Mnunuzi mwingine, Bw John Macharia Maina, alieleza kuwa alijaribu kujenga lakini jengo lilibomolewa na watu wasiojulikana.

Kwa uamuzi huu, familia ya Kamotho imepoteza rasmi umiliki wa shamba hilo kwa msingi kwamba haikuwahi kuchukua hatua ya kulitwaa kwa zaidi ya miaka 12, muda unaotambuliwa kisheria kuruhusu madai ya umiliki wa muda mrefu.