• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Familia yadai marehemu aliwaletea ndoto kusaidia kumpata nyoka muuaji

Familia yadai marehemu aliwaletea ndoto kusaidia kumpata nyoka muuaji

NA FRIDAH OKACHI

FAMILIA moja katika kijiji cha Musanyi kilichoko eneo la Isukha Mashariki, kwenye mpaka wa kaunti za Nandi na Kakamega inaomboleza kumpoteza mmoja wao aliyeumwa na nyoka.

Boniface Lukonya Lutenya,48, alifariki saa mbili tu baada ya kuumwa na nyoka.

Familia ya marehemu iliambia Taifa Leo kwamba matibabu ya haraka hayakupatikana.

Dadake marehemu, Bi Florence Lutenya, alisema Jumanne kwamba anashuku kaka yake aliaga dunia kutokana na sumu ya nyoka kwani alikosa kutafuta huduma za haraka ili kuzuia sumu hiyo kusambaa.

“Kabla kakangu akumbane na mauti alitueleza alimkanyaga nyoka ambaye alimuuma. Alituambia aliketi pahala fulani kichakani akitafakari jambo la kufanya. Baadaye alikuja nyumbani baada ya saa moja na kutufahamisha kilichojiri,” akaeleza Bi Lutenya.

Bi Lutenya alisema familia ilimpeleka katika zahanati ambapo alipewa barua ya kupelekwa katika hospitali ya Kapsabet.

“Hakuweza kupokea huduma ya kwanza na tukaagizwa tumpeleke katika hospitali nyingine. Hapo sasa alikuwa amemaliza saa mbili hivi. Tukiwa kwenye harakati ya kutafuta gari la kumsafirisha hadi Kapsabet aliaga dunia,” aliongeza Bi Lutenya.

Jumanne asubuhi, kaka yake mwingine, Bw Josphat Lutenya, aliambia familia kuwa marehemu alizungumza naye kwenye ndoto na kumfahamisha alipo nyoka huyo muuaji.

Wanakijiji waliandamana hadi kwenye msitu wa Kakamega, sehemu alipoumiwa marehemu, na kuanza kumtafuta nyoka huyo.

“Hatukuchukua muda kumpata maana kaka yangu alinifahamisha kwenye ndoto sehemu alipokuwa nyoka huyo. Nilitaka jamii imuue jinsi aliniagiza kwenye ndoto,” akasimulia Josphat.

Baada ya kumpata nyoka huyo, wanakijiji hao walimweka kwenye gunia na kumbeba hadi nyumbani kwa familia ya marehemu na kumuua.

“Tulimpata nyuka huyo hiyo sehemu aliyomuumia ndugu yangu. Ni nyoka ambaye hupatikana kwenye shimo au kwenye sehemu ya mti uliokatwa. Tulimleta nyumbani na kumua jinsi marehemu alivyonielezekeza kwenye ndoto,” aliongeza.

Marehemu atazikwa Jumamosi ijayo.

Chifu wa Musanyi Bw Wycliffe Ambani, alionya wakazi wa eneo hilo na kuwataka kuwa makini wanapoingia kwenye msitu huo.

Aliwaambia wawe macho wanapokanyaga kwa msitu wowote na maeneo ya nyasi nyingi.

Akizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu, Bw Ambani alidokeza kuwa visa kadhaa vya nyoka kuvamia wenyeji vimetokea.

Alitoa wito kwa Wizara ya Afya kuweka dawa ya kupunguza sumu ya nyoka kwenye zahanati zilizoko karibu.

“Visa hivi vimeongezeka siku za hivi karibuni. Tatizo kuu hakuna dawa kwenye zahanati zetu. Wengi wanapewa barua kwenda hospitali zilizo mbali na kusababisha maafa,” alisema Bw Ambani.

Sumu ya nyoka husambaa kwenye mwili wa binadamu kupitia mfumo wa maji katika mwili unaoitwa lymphatic.

Nyoka wengi huacha sumu aina ya Venom kwa mwili wa binadamu na inaweza kusababisha mwili kufura, tishu kuharibika na hata kusababisha kifo endapo mwathiriwa hatapata matibabu haraka upesi.

  • Tags

You can share this post!

Omtatah awasilisha kesi kupinga Mswada wa Fedha wa 2024

Magavana wa zamani kusomewa ‘dhambi’ zao mbele...

aaronmalcolm48