Habari za Kitaifa

Familia yahofia hali ya kijana wao aliyetekwa kwa kuchapisha picha kuhusu Ruto

Na CECIL ODONGO December 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

FAMILIA moja Kaunti ya Embu imekumbwa na wasiwasi baada ya mwanao kutekwa nyara na wanaume wanne waliovalia kofia huku visa vya utekaji nyara vikiendelea kuongezeka nchini.

Mnamo Desemba 21, Billy Munyiri Mwangi, 24 ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu alikuwa kwenye kinyozi katika mji wa Embu, akisubiri kunyolewa wakati gari aina ya pick-up lenye rangi nyeupe liliposimamishwa ghafla.

Wanaume wanne waliovalia kofia za kufunika nyuso zao wanaoshukiwa kuwa maajenti wa usalama wa serikali walishuka, wakamkamata Bw Mwangi na kumpeleka kwenye gari, jambo lililowashangaza waliokuwa karibu.

Bw Mwangi alipotaka kujua ni kwa nini alikamatwa, watu hao wakamjibu, “utajua baadaye.”

Kisha watu hao walimfungia Bw Mwangi ndani ya gari na kuondoka kwa mwendo wa kasi.

Kulingana na familia mtoto wao alichukuliwa Jumamosi mwendo wa saa tatu usiku.

“Mwana wetu alikuwa katika duka la kinyozi akisubiri zamu yake ya kunyolewa ndipo watu hao walifika ghafla na kumchukua bila kutoa sababu zozote,” akasema Bi Regina Wairimu, mamake Mwangi.

Bi Wairimu alisema alikuwa nyumbani alipopokea habari kwamba mwanawe alinaswa na kusafirishwa hadi mahali pasipojulikana.

“Tukio hilo limetuacha na maswali tele kuhusu aliko mwana wetu. Ikiwa serikali imehusika, nataka mwanangu arejeshwe nyumbani akiwa hai. Na kama amefanya kosa nipo tayari kuomba radhi kwa niaba yake,” alisema Bi. Wairimu huku akilia.

Naye Gerald Karicha, babake Mwangi alisema, “Nina uchungu kufuatia kutekwa nyara kwa mwanangu.”

Anasema alimpigia mwanawe simu mwendo wa saa tatu usiku ila alikuwa mteja.

“Nilitaka tutazame soka pamoja nyumbani. Hivyo nilimpigia simu saa tatu usiku lakini simu yake ilikuwa imezimwa, nikawa na mashaka kuwa huenda kuna shida. Tulianza kumtafuta na tukaripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Embu,” akasema Bw Karicha.