Habari za Kitaifa

Familia yaomba huruma huku polisi wakipanga kushtaki waliorushia Rais kiatu kwa uhaini

Na GEORGE ODIWUOR May 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANAUME  wanne waliokamatwa kuhusiana na tukio ambalo Rais William Ruto alirushiwa kiatu katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kuria Magharibi, Kaunti ya Migori, huenda wakakabiliwa na mashtaka ya uhaini, hatua ambayo imezua taharuki miongoni mwa familia zao na wakazi wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa hati ya kiapo iliyowasilishwa katika Mahakama ya Kehancha na Afisa Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wa eneo hilo, John Njogu, wanaume hao wanakabiliwa na mashitaka ya uhaini kinyume na kifungu cha 40(1)(a)(i)(3) cha Kanuni ya Adhabu.

Ikiwa watapatikana na hatia, adhabu ya kosa hilo ni kifo.

Washukiwa hao Nicholas Mwita, Emanuel Chach, Paul Mutongori na Hezron Moherai, wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kehancha huku uchunguzi ukiendelea.

Hakimu Mkuu John Paul Nandi, alikubali ombi la polisi la kuwazuilia kwa siku 14 hadi Aprili 25, 2025.

Katika video iliyosambaa mitandaoni, Rais Ruto anaonekana akiepuka kiatu kilichotupwa kwake, jambo lililoibua hisia mseto kuhusu usalama wake.

Sehemu ya hati ya kiapo ilisema: “Wakati wa hotuba ya Mheshimiwa Rais katika hafla ya uzinduzi wa Nyumba za bei nafuu katika mji wa Kehancha, vurugu zilianza miongoni mwa umati na kiatu kilirushwa kuelekea kwake, kilimpiga mkono, na kusababisha taharuki miongoni mwa waliohudhuria.”

Mpelelezi Njogu alisema washukiwa walitambuliwa kupitia video zilizorekodiwa na kusambazwa mtandaoni. “Kuna haja ya muda zaidi kufanya uchunguzi kutokana na uzito wa kosa hili,” alieleza.

Aidha, DCI inapanga kuwashitaki kwa kosa la kusababisha vurugu kinyume na kifungu cha 95(1)(b) cha Kanuni ya Adhabu. Njogu aliongeza kuwa washukiwa hawajulikani wanakoishi na hivyo ni hatari kuachiwa kwa dhamana kwani wanaweza kutoroka.

Familia ya Paul Mutongori imejitokeza kumtetea, ikisema anasingiziwa. Mama yake, Esther Marwa, alisema: “Mwanangu si mhalifu. Hajawahi kukamatwa wala kuhusika katika uhalifu. Nilimlea katika maadili na hakuwahi kuvutiwa na siasa.”

Kulingana na mama huyo, Paul, ambaye ni mchimbaji wa dhahabu mwenye umri wa miaka 18, hakuwa sehemu ya kundi lililorusha kiatu.

“Alikamatwa baadaye akiwa kwenye baa na hakuambiwa sababu ya kukamatwa kwake. Alikiri tu kuwa alikuwa kwenye hafla ya rais, lakini hakuwa karibu na waliofanya vurugu,” alisema.

Dada yake Paul, Rose Swagi, alisema mama yao alipoteza fahamu alipopata taarifa kuhusu kukamatwa kwa mwanawe. “Tuliweza kumpatia huduma ya kwanza, lakini hali hiyo inaweza kumletea matatizo ya kiafya,” alisema kwa wasiwasi.

Rafiki yake Paul, Emmanuel Mananga, alisema: “Paul si mtu wa ghasia. Hajawahi kuwa mkorofi na ni mtu wa amani. Hawezi kuwa alihusika.”

Wakazi wa Kuria waliungana na familia hizo wakisema kwamba eneo hilo lina uhusiano mzuri na Rais Ruto. Mbunge wa Kuria Mashariki, Marwa Kitayama, alisisitiza kuwa tukio hilo halikuwa na nia mbaya, bali lilitokea kutokana na msisimko wa vijana waliotaka kumuona Rais.