Habari za Kitaifa

Familia yataka mwanaharakati Mwabili Mwagodi aliyetekwa akiwa Tanzania aachiliwe huru

Na KEVIN CHERUIYOT July 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mwanahabari kutoka Kenya, Bi Isabella Kituri, ambaye ni dada wa mwanaharakati  Mwabili Mwagodi, ametoa wito kwa serikali ya Kenya kumsaidia kumtafuta nduguye aliyeripotiwa kutoweka nchini Tanzania tangu Jumatano.

Bi Kituri ameomba ubalozi wa Kenya nchini Tanzania kuingilia kati katika juhudi za kumtafuta Bw Mwagodi, baada ya madai kuibuka kwamba huenda alikamatwa kwa sababu ya kukosoa serikali ya Rais William Ruto.

Akizungumza na wanahabari, Bi Kituri alisema familia yao imeingiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kutoweka kwa ndugu yao, na amesisitiza kuwa Bw Mwagodi anapaswa kuachiliwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani salama.

“Kama kuna lolote alilofanya, basi afikishwe mahakamani kwa njia ya wazi kupitia mfumo wa haki. Naomba serikali ya Kenya na Tanzania kutumia taratibu za kisheria kushughulikia jambo hili,” alisema Bi Kituri mbele ya waandishi wa habari.

Bw Mwagodi, ambaye anaripotiwa kutoweka tangu Jumatano, amekuwa mstari wa mbele katika kuikosoa serikali kuhusu misaada yake kwa makanisa.

“Tunataka tu wale wanaomzuilia wajue kuwa tunafahamu alikopelekwa, na kwamba watabeba lawama. Haki lazima itendeke,” aliongeza dada yake.

Alisema nduguye anatumia haki yake ya kikatiba ya kutoa maoni, hususan kuhusu uadilifu wa taasisi za kidini.

Bw Mwagodi alikuwa akifanya kazi katika mkahawa mmoja Kigamboni, Dar es Salaam alipotoweka.

Pia alikuwa mmoja wa wanaounga mkono maandamano ya kizazi cha Gen Z, akitumia mitandao yake ya kijamii kuelezea kutoridhika kwake na baadhi ya sera za serikali.

Kwa mujibu wa mwanaharakati wa haki za binadamu, Bw Hussein Khalid, Bw Mwagodi huenda amekuwa mhasiriwa mwingine wa utekaji, hali inayozua wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa wanaharakati wa Kenya walioko Tanzania.

Hili linajiri huku kukiwa na wito wa kutolewa kwa ripoti kamili kuhusu mwanaharakati Boniface Mwangi na mwenzake kutoka Uganda, Agather Atuhaire, waliodaiwa kutekwa nyara na kudhulumiwa kingono.

Mnamo Mei, kiongozi wa Chama cha People’s Liberation Party na waziri wa zamani wa haki nchini Kenya, Martha Karua, pamoja na wanaharakati wengine, walikamatwa na baadaye kufurushwa Tanzania kwa sababu ambazo hazikufichuliwa.

Walikuwa wamepanga kufika mahakamani kuhudhuria kesi ya kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, lakini mipango hiyo ilizimwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.