Habari za Kitaifa

Faye amteua mwandani wake kuwa Waziri Mkuu muda mfupi baada ya kuapishwa

April 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

DAKAR, Senegal

Na MASHIRIKA

RAIS mpya wa Senegal Bassirou Diomaye Faye amemteua mwanasiasa shupavu na mwandani wake, Ousmane Sonko kuwa Waziri Mkuu katika uteuzi wake wa kwanza baada ya kuingia mamlakani rasmi.

Faye, 44, alifanya uteuzi huo Jumanne dakika chache baada ya kulishwa kiapo huku akiahidi kutekeleza mabadiliko katika mfumo wa uongozi wa taifa hilo.

Kiongozi huyo, ambaye ameshika rekodi kama mtu wa umri wa chini zaidi kuwa kuchaguliwa kuwa Rais nchini Senegal, amechukua hatamu za uongozi kutoka kwa Macky Sall, hasidi mkubwa wa Sonko.

Akiongea baada ya uteuzi wake, Sonko aliahidi kumpa, Faye majina ya watu atakaopendekeza kwa uteuzi kuwa mawaziri ili aidhinishe.
“Sitamwachia Rais wajibu huu muhimu na mzito. Nitautekeleza haraka iwezekenavyo,” Sonko akaeleza.

Faye alilishwa kiapo mbele ya mamia ya maafisa wa serikali na marais kadhaa wa mataifa ya Afrika ndani ya ukumbi wa exhibition centre katika mji mpya wa Rais huyo, ambaye zamani alifanyakazi katika mamlaka ya ukusanyaji ushuru, alimshinda Amadou Ba aliyeungwa mkono na Sall katika awamu ya kwanza kwa kupata asilimia 54 ya kura.

“Matokeo ya uchaguzi huo yalionyesha uwepo wa haja kubwa ya mabadiliko nchini mwetu,” Faye akasema baada ya kulishwa kiapo katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na wake zake wawili.

Miongoni mwa marais waliohudhuria hafla hiyo ni; Rais wa Nigeria Bola Tinubu na mwenzake wa Ghana Akufo-Addo.

Pia alikuwepo Mwenyekiti wa Tume ya Umma wa Afrika (AUC) Moussa Faki Mahamat.

Viongozi wa kijeshi wa nchi za Burkina Faso, Mali na Niger pia walituma wawakilishi.

Mabadiliko hayo ya uongozi nchini Senegal yalileta afueni mpya katika nchi hiyo ambayo imezongwa na misukosuko ya kisiasa kwa miaka mitatu.

Hali hiyo ilionekana kama pigo katika rekodi ya nchini hiyo ambayo ni kipekee lenye demokrasia pevu Afrika Magharibi.

Eneo hilo limeshuhudia mapinduzi ya kijeshi huku watawala wapya wakikatiza uhusiano na mataifa ya Magharibi na kuegemea Urusi.

“Senegal itakuwa nchi ya matumaini, yenye amani, yenye mfumo huru wa haki na demokrasia thabiti,” Faye akasema.

Kiongozi huyo ambaye, pamoja na Sonko, walifungwa jela na utawala wa Sall na kuchiliwa siku 10 tu kabla ya uchaguzi, aliahidi kutoongozwa na ukabila anapojenga uchumi wa taifa hilo.

Mamilioni ya raia wa Senegal walipiga foleni kwa saa kadhaa kushiriki upigaji kura mnamo Machi 24, mwaka huu.

Hii ni baada ya serikali ya Sall kujaribu kuahirisha uchaguzi huo kutoka Februari hadi Desemba lakini ikalemewa na presha kutoka kwa viongozi wa upinzani na raia.

Umaarufu wa Sall ulishuka zaidi wakati wa muhula wake wa pili uongozini kutokana na kudorora kwa uchumi, hatua ya serikali kuwadhulumu viongozi wa upinzani na hofu kwamba angeshinikiza mabadiliko ya katiba ili awanie urais kuongoza kwa muhula wa tatu.