Fidia ya wahanga wa maandamano yaibua upinzani: ‘Maisha ya mtu ni milioni ngapi?’
UAMUZI wa Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga kuzindua mpango wa kuwalipa fidia wahanga wa maandamano umeibua wasiwasi kuhusu utekelezaji wake na mitazamo ya kisiasa.
Wanaokosoa mpango huo wanasema kuwa ungetekelezwa kupitia mwongozo wa kuwalinda waathiriwa badala ya kuanzishwa kama sehemu ya makubaliano ya kisiasa kati ya Rais Ruto na Bw Odinga.
Kwa mujibu wa Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa, Bw John Okumu, siasa ambazo zimezingira kutolewa kwa fidia, kunatokana na shinikizo kutoka kwa Raila ambaye amekuwa akiongoza maandamano nchini.
“Bw Odinga ni kati ya waathiriwa ambao wamelipwa fidia baada ya kuingia kwenye Serikali Jumuishi. Hii ni licha ya kuwa serikali hii imekuwa ikikandamiza na kuwadhulumu vijana wa Gen Z ambao wanaandamana wakitaka uongozi bora,” akasema Bw Okumu.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa UDA, Bw Cleophas Malala ambaye kwa sasa ni naibu kiongozi wa DCP, pia amepinga mpango wa kuwalipa fidia waathiriwa wa maandamano.
“Tunataka kujua thamani ya maisha ambayo yamepotezwa kupitia dhuluma inayofanikishwa na serikali. Tuseme familia italipwa Sh10 milioni kwa kupoteza mwanao kwenye maandamano, wanaotaka fidia hii ilipwe wapo radhi watoto wao wauawe ili wapate pesa hizo?” akauliza.
“Tuonyeshe sheria ambayo inathamini maisha na ile ambayo inampa Dkt Ruto na Bw Odinga uwezo kuamua mwaathiriwa wa maandamano. Wanataka kutumia mamlaka ambayo hawana,” akasema Bw Malala.
Ili kufanikisha mchakato wa kulipwa kwa fidia hii, Rais Ruto alimteua mwanasiasa Profesa Makau Mutua aongoze shughuli hiyo kwa siku 120.
Kazi ya kamati inayoongozwa na Profesa Makau itakuwa kutoa mwongozo wa kulipwa kwa familia za waliouawa au kujeruhiwa wakati wa maandamano kati ya 2017-2025. Pia waliopoteza mali yao hasa kibiashara watalipwa fidia na serikali kulingana na ushahidi ambao utawasilishwa.
Hata hivyo, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, alisema waathiriwa wa dhuluma za serikali hawawezi kuhesabiwa tu kutoka 2017-2025.
“Lazima tuwafidie wote ambao wamedhulumiwa na serikali kwa usawa. Kuna wale wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/08 na pia kuna wale ambao waliteswa nyakati za kupigania uhuru,” akasema Bw Gachagua.
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka naye amepinga mpango huo akisema ni kejeli kutoka kwa serikali.
“Huwezi kuongoza serikali ambayo imejikita katika utekaji nyara, mauaji ya kiholela na mateso kisha usema unawalipa fidia uliowadhulumu,” akasema.
Alisisitiza kuwa polisi waliowapiga risasi raia na makamanda wao lazima washtakiwe kabla ya fidia zozote kulipwa.
Bw Jonah Kariuki ambaye ni babake muuzaji wa bakora Boniface Mwangi ambaye alipigwa risasi wakati wa maandamano Nairobi mnamo Julai 16, 2025 , naye amesema pendekezo la kuwalipa fidia linabagua.
“Huwezi kutuua kisha uje kwa familia zetu na kusema unatulipa. Kuna thamani gani ya maisha ya binadamu iwapo hali ni hii? Serikali inastahili kuwasikiza raia wake na isiwaue,” akasema Bw Kariuki kwenye mahojiano.