Fumbo kuhusu ajali iliyochukua uhai wa Jirongo; je, kuliendaje?
ALIYEKUWA Mbunge wa Lugari, Bw Cyrus Jirongo, huenda alifariki dunia kutokana na majeraha aliyopata katika ajali ya gari iliyotokea Desemba 13, lakini maswali kadhaa ambayo hayajajibiwa yamewaacha wengi, hususan familia na marafiki zake, wakiendelea kutafuta ukweli kamili kuhusu kifo chake.
Miongoni mwa maswali yanayozua sintofahamu ni sababu ya marehemu kuelekea Naivasha, hatua ya wachunguzi kukataa kuweka wazi video za CCTV za ajali hiyo, kimya cha abiria 67 waliokuwa ndani ya basi la Climax Coaches lililogongana na gari la marehemu, pamoja na jinsi eneo la ajali lilivyoshughulikiwa.
Masuala haya yamezua tetesi na maswali mengi kuhusu chanzo cha kifo chake kwa karibu wiki moja sasa.
Mtaalamu wa upasuaji wa maiti wa serikali, Dkt Johansen Oduor, akishirikiana na madaktari walioteuliwa na familia na marafiki wa marehemu, Joseph Ndung’u, Bernard Midia na Martin Wanyoike, alisema Jumatano kuwa majeraha yaliyosababisha kifo cha Bw Jirongo yalionekana kufanana na yale yanayotokana na ajali ya barabarani.
Ripoti ya upasuaji wa maiti imekuwa msingi muhimu kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), ambayo Jumanne ilianzisha uchunguzi rasmi kuhusu kifo hicho.
Katika taarifa yake, DCI ilisema ilimhoji dereva wa basi la Climax Coaches, Tyrus Kamau Githinji, pamoja na wafanyakazi wa kituo cha mafuta cha Eagol ambacho marehemu alitoka muda mfupi kabla ya ajali.
Akizungumza mwishoni mwa taarifa yake, Dkt Oduor alisema kuwa kikosi chake kilichukua sampuli zaidi kwa uchunguzi wa kina kutokana na maswali ambayo bado hayajajibiwa.
“Bw Jirongo alifariki kutokana na majeraha mabaya sana ya kifua yaliyosababishwa na ajali, kama ilivyobainishwa wazi na madaktari. Uchunguzi huu wa maiti ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea. Tumekamilisha uchunguzi wa awali, lakini pia tumechukua sampuli kwa uchambuzi zaidi kutokana na wasiwasi unaoendelea,” alisema Dkt Oduor.
Aliongeza kuwa sampuli hizo zitachunguzwa na Mwanakemia Mkuu wa Serikali na pia mtaalamu aliyeteuliwa na familia, huku sampuli za DNA zikichukuliwa. Aliwataka wananchi wawe na subira uchunguzi ukiendelea.
Athari za ajali hiyo zilisababisha majeraha makubwa kwenye kifua, mgongo na tumbo la marehemu, na alifariki kabla ya kuondolewa kwenye gari.
Dkt Ndung’u alisema mwili ulikuwa na majeraha mengi, ikiwemo mifupa kuvunjika mikononi na miguu yote miwili, mbavu nyingi kuvunjika, moyo kupasuka pamoja na mishipa yake, damu kujaa kwenye kifua na tumbo, ini kuathirika, na uti wa mgongo kukatika katika sehemu ya kifua.
Madaktari Midia na Wanyoike pia walikubaliana na matokeo hayo.
Aliyekuwa Seneta wa Vihiga, George Khaniri, ambaye ni miongoni mwa watu wa mwisho kuonana na kuzungumza na marehemu, alikuwa wa kwanza kuibua maswali kuhusu mazingira ya kifo chake, akiuliza alichokuwa akifanya Karai, ambako gari lake aina ya lMercedes-Benz liligongana na basi la Climax.
Bw Khaniri alisema alizungumza na marehemu saa tano usiku kabla ya ajali, akimkumbusha kuhusu mkutano muhimu uliopangwa siku iliyofuata, na marehemu akamwambia alikuwa akielekea nyumbani Gigiri.
Hata hivyo, saa tatu baadaye alitangazwa kuwa amefariki, umbali wa kilomita 76 kutoka nyumbani kwake.
MERCY KOSKEI, STEVE OTIENO, KAMORE MAINA NA NYABOGA KIAGE