Habari za Kitaifa

Gachagua afyatuka rasmi kujaribu kumwondoa Ruto afisini

Na KEVIN CHERUIYOT May 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais, Rigathi Gachagua sasa ameanzisha mikakati rasmi ya kumwondoa afisini Rais William Ruto 2027 kwa kutaja rasmi chama chake cha kisiasa atakachokitumia kufanikisha azma hiyo.

Bw Gachagua anapanga kukitumia chama cha Democracy for Citizen Party (DCP) kusuka muungano na vinara wa vyama vingine vya upinzani kudhamini mgombeaji mmoja wanayemtarajia kumfanya Dkt Ruto aandikishe historia kama rais wa kwanza nchini kuhudumu muhula mmoja pekee.

Akihutubu jijini Nairobi jana alipoongoza shughuli ya kutambulisha chama hicho kwa Wakenya, mbunge huyo wa zamani wa Mathira alieleza kuwa kitaendeleza matakwa ya raia.

“Hii ndio maana kauli mbiu ya chama chetu ni ‘Sikiza Wakenya’ au ‘Sikiza Ground’,” akasema.

“Hata wale wengine wakija kule Murang’a na sehemu nyinginezo wakiahidi kufanya hili na lile, muwaambie wasikize ground, yaani wazingatie matakwa ya wananchi mashinani,” Bw Gachagua akaeleza akionekana kuashiria kuwa mizizi ya chama hicho iko Mlima Kenya.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa DCP kilichosajiliwa rasmi mnamo Februari 3, mwaka huu, ni chama cha kitaifa huku nadhifa za uongozi wake zikisambazwa maeneo yote ya nchi na kwa umri wote, wakiwemo vijana wa kizazi cha Gen Z.

Ili kuthibitisha kauli hiyo, Bw Gachagua alitaja orodha ya viongozi wa muda wa DCP, ambao ni watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi.

Uzinduzi wa chama hicho ulikumbwa na vurugu baada ya watu wasiojulikana kuvamia hafla hiyo. Tukio hilo linaongeza msururu wa matukio ya ghasia za kisiasa zinazoshuhudiwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Wavamizi hao waliwashambulia baadhi ya waliohudhuria hafla hiyo fupi katika ofisi za chama hicho mpya zilizoko Lavington, Nairobi.

Walilizingira eneo hilo na kuwapiga baadhi ya waliohudhuria kabla ya walinzi wa Gachagua kuwatawanywa kwa kufyatua risasi hewani.

Naibu Rais Kithure Kindiki alilaani tukio hilo vikali, akisisitiza kuwa taifa linapaswa kudumisha uvumilivu wa kidemokrasia na siasa za hoja.

“Matusi, vurugu na kauli za kugawanya watu hazina nafasi katika jamii yetu. Tunawajibika kwa vizazi vya sasa na vijavyo kujenga taifa lenye amani, heshima kwa kila mmoja hata tunapokosa kuelewana,” alisema Profesa Kindiki.

Tukio la Alhamisi si la kwanza.

Mnamo Aprili 6, 2025, tukio kama hilo lilitokea katika kanisa la PCEA Mwiki kwenye hafla iliyohudhuriwa na Gachagua.

Pia, Novemba iliyopita, alikimbia kutoka kwa mazishi Kiambu baada ya kushambuliwa na umati wenye hasira.

Katika uzinduzi huo, Gachagua alitangaza kuwa chama chake kitaandaa kongamano kubwa la kisiasa Juni 4, 2025 kuzinduliwa rasmi.

Alijitambulisha kama kiongozi wa kitaifa wa chama hicho huku akimtaja aliyekuwa Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala kama naibu wake.