Gachagua alia majasusi wa serikali wanamuandama kila anakoenda
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amelalamika kuwa serikali inamuandama hata baada ya kuondolewa mamlakani.
Bw Gachagua alidai kuwa majasusi wa serikali wamekuwa wakimfuata kila anapoenda wakitumia magari yasiyo rasmi.
Maafisa wa usalama katika magari yasiyo rasmi wamekuwa wakinifuata popote ninapoenda. Wanaegesha( gari) kwenye lango la makazi yangu Nairobi, wakichunguza wageni wangu wote, na wananifuata kila ninapotoka nyumbani, hata hadi nyumbani kwangu huko Nyeri,” Bw Gachagua alisema kwenye taarifa kupitia mitandao yake ya kijamii.
“Jumapili iliyopita, gari la saluni lililokuwa limeegeshwa kwenye lango la makazi yangu lilinifuata hadi Kanisa la PCEA Kerarapon, lilinifuata nilipoenda kula chakula cha mchana na kurudi nyumbani! Niliposaka maelezo kutoka NTSA, niligundua kuwa nambari zake zaq usajili ni za lori,” alieleza na kuambatisha picha ya gari hilo na cheti alichodai ni cha usajili kutoka NTSA.
“Ufuatiliaji huu na vitisho wa Wakenya vilishuhudiwa mara ya mwisho enzi za Special Branch (lililokuwa shirika la ujasusi enzi za utawala wa chama cha Kanu” wakati wa miaka 24 ya utawala mbovu wa Moi!
Kwa mara nyingine, Bw Gachagua alisema anahofia maisha yake yamo hatarini.
“Katika zama hizi za mauaji ya kiholela, utekaji nyara na kutoweshwa kwa nguvu na vyombo vya serikali , nimeona ni muhimu kuwaambia Wakenya unyanyasaji na vitisho ninaopitia, na kuwafahamisha kuiwajibisha serikali iwapo nitadhuriwa na maajenti wa serikali,” alisema.
Aliitaka serikali ikome kuwamwandama akisema ashakuwa raia wa kawaida baada ya kutimuliwa mamlakani.
“Naomba serikali iniache. Nilifukuzwa ofisini, na sasa ninapaswa kuruhusiwa kufurahia amani yangu kama raia wa kawaida,” alisema.