Habari za Kitaifa

Gachagua alia viongozi walilipwa kutibua mkutano wake na kumuaibisha Nyeri

Na MERCY MWENDE, CECIL ODONGO January 9th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amewashutumu baadhi ya viongozi wa kutoka Nyeri akidai walipanga njama na Rais William Ruto kumzuia kuandaa mkutano wa kisiasa mjini Nyeri mnamo Alhamisi.

Bw Gachagua alisikitika kuwa baadhi ya viongozi aliowasaidia kutwaa viti vya kisiasa, ndio sasa wanatumiwa kumpiga vita na wamesaliti jamii ya Mlima Kenya.

Alidai viongozi hao walipewa pesa ili kuwalipa vijana wavuruge mkutano wake Nyeri.

Alitaja kuendelea kuhangaishwa kwake hata kwenye ngome yake ya kisiasa kama jambo lisilofaa kwa sababu alisimama na Rais William Ruto mnamo 2022.

“Rais amewapa viongozi wa hapa pesa ili wavuruge mkutano wangu ndipo nisihutubie wakazi wa hapa. Watoto wetu wamelipwa wavuruge mkutano wangu,” akasema Bw Gachagua akihutubu kwenye mkutano huo uliofahamika kama “Karibu Nyumbani Riggy G”.

Bw Gachagua aliwataka vijana wajiepushe kutumika na wanasiasa, akisema ni vibaya sasa vijana wa Nyeri wanatumika kuwavamia wazazi wao.

Kiongozi huyo wa DCP alisema viongozi kutoka Nyeri ambao wanamuunga mkono Rais Ruto hawatachaguliwa 2027, kwa sababu wameasi maslahi ya jamii.

Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga ambaye alikuwa ameandamana na Bw Gachagua alisema walipokea habari za kijasusi kuhusu mpango wa kutibua mkutano huo.

Bw Kahiga alisema aliyekuwa naibu rais ndiye kigogo wa siasa za Mlima Kenya na akasema wanasiasa wote wanastahili waruhusiwe kufanya kampeni bila wahuni kukodishwa kuwavuruga.

Viongozi walioandamana na Bw Gachagua walikashifu tukio ambapo vijana waliokuwa wamejihami kwa bakora na panga wakiandamana na maafisa wa polisi, walionekana wakitembea mjini Nyeri.

Walisema tukio hilo lilionyesha kwamba ghasia dhidi ya mbunge huyo wa zamani wa Mathira zilikuwa zimedhaminiwa na serikali.

Ingawa Bw Gachagua aliratibiwa kuwahutubia wafuasi wake saa 10 jioni, mkutano ulianza saa 11 jioni.

Baadhi ya vijana waliokuwa wamejihami walionekana wakitoa ulinzi katika sehemu ya kuingia mji huo.

Wafanyabiashara nao walifunga biashara zao kwa hofu ya ghasia kutokea huku wenyeji waliokuwa wakipiga picha na kuchukua video ya vijana waliojihami, wakitishiwa.

Kabla kufika mkutanoni, Bw Gachagua alikuwa amechapisha kwenye mtandao wake wa X jinsi vijana waliojihami walikuwa wakizurura mjini Nyeri na kupanga kutibua mkutano wake.

“Nilifikiria Rais alitoa amri kuwa wahuni hawafai waruhusiwe wawahangaishe Wakenya mahali popote,” akaandika na kutundika video ya vijana waliojihami.