Habari za Kitaifa

Gachagua atangaza chama cha Mlima Kenya ni UDA

May 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI 

MALUMBANO ya kisiasa katika Mlima Kenya yamezidi kuchacha huku Naibu Rais Rigathi Gachagua akiyataja kuwa sarakasi na upuzi.

Bw Gachagua ameonekana katika siku za hivi majuzi akipigwa miereka ya kisiasa na baadhi ya wanasiasa wenzake ambao baadhi yao hata wamependekeza afutwe kazi.

Aidha, wengine wamemtaka Rais William Ruto kumteua mwingine kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa 2027 na pia atemwe nje katika hesabu ya kurithi urais 2032.

Naye Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria amesema vita hivyo vya kiubabe vimepambwa katika mazingira ya ujinga.

Alirejelea kisa ambapo katika kambi ya wakimbizi wa mafuriko ya Ngutu katika Kaunti ya Murang’a Bw Gachagua na Bw Nyoro walionekana kushindana kuomboleza watu saba ambao waliaga dunia.

Mnamo Aprili 30, 2024, Bw Nyoro alifika wa kwanza akiandamana na baadhi ya viongozi wa Murang’a lakini muda mfupi baada yake kuondoka, Bw Gachagua akafika akiandamana na wanasiasa kutoka Kaunti ya Nyeri.

Ni katika ziara hiyo ambapo Bw Gachagua alilia hadharani kwamba huwa na mapenzi na wenyeji lakini huwa anakosa wa kumwalika na kumlaki.

“Sasa, niliona suala la kufedhehesha ambapo pale Murang’a walionekana wakibishania kuomboleza. Watu wamekufa na kile tuliona ni watu kushindana eti ni nani atafika na ndege kwanza,” Bw Kuria akasema.

Aliongeza kwamba “ndege moja ikitua eneo hilo la wakimbizi ndio nyingine ilikuwa inapaa angani kuelekea huko… huo ni ujinga wa kiwango gani!” Kuria akashangaa.

Akiwa katika Kanisa la Anglikana (ACK) la Kamiti katika Kaunti ya Kiambu, Bw Gachagua alisema kwamba “mimi ndiye niliye na cheo kikubwa zaidi Mlima Kenya na sina wakati wa siasa za uigizaji, sarakasi na upuzi”.

Gavana wa Kiambu Bw Kimani Wamatangi alisema kwamba “kwa sasa kile tunafaa kuzingatia ni huduma kwa wananchi na kila kiongozi ahudumu katika wadhifa aliopewa”.

Aliwataka wanasiasa waelewe kwamba Bw Gachagua kwa sasa ndiye amepewa jukumu la kuwa Naibu Rais na yuko katika afisi hiyo hadi 2027.

“Wewe Naibu Rais utaulizwa na wapigakura uwaelezee ni yapi uliwatimizia katika wadhifa huo na utawajibu wewe mwenyewe huku nasi katika nyadhifa zetu tukiwajibishwa mtihani sawa na huo katika majukumu tuliyo nayo,” Bw Wamatangi akasema.

Bw Gachagua alisema yuko na kazi ya kuwaunganisha wenyeji wa Mlima Kenya ndani ya serikali ya Ruto hadi 2032 huku chama chao kikiwa ni United Democratic Alliance (UDA).

Kumekuwa na tetesi Mlima Kenya kwamba eneo hilo linahitaji chama cha nyumbani ili kutumika katika kung’ang’ania minofu ya serikali.

“UDA ni chama chetu kwa wingi wa kura na ni lazima tukidhibiti na tujiweke ndani kwa wingi kupitia uchaguzi wa mashinani tunaoendeleza,” akasema Bw Gachagua.