Habari za Kitaifa

Gachagua atoroshwa, wahuni wakimvamia kanisani Othaya, kuhutubia taifa

Na GITONGA MARETE January 25th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

WAFUASI wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua walilazimika kumtorosha hadi eneo salama Jumapili baada ya polisi kurusha vitoza machozi kwenye kanisa alilokuwa amehudhuria ibada Kaunti ya Nyeri.

Kwa mujibu wa waumini, polisi walifika Kanisa la ACK Witima na kurusha vitoza machozi huku waliokwepo wakikimbia kujinusuru.

Watoto na akina mama ambao walikuwa wamehudhuria ibada katika kanisa hilo walilemewa na moshi wa vitoza machozi. Pia kulikuwa na wahuni nje ya kanisa ambao waliyapiga magari kwa mawe.

“Baadhi ya wahuni walikuwa wamevalia jaketi na walikuwa na mtungi wa gesi za vitoza machozi,” akasema  muumini mmoja.

Bw Gachagua mwenyewe alisema polisi waliharibu gari lake katika Kanisa la Witima ACK ambako alikuwa amejumuika na waumini.

Kamanda wa Polisi wa Nyeri Kipchirchir Too alisema kuwa alipopokea habari hizo, hakukuwa na afisa yeyote kanisani humo.

“Maafisa wangu hawakuwa pale lakini nimewatuma wanane kuchunguza kile kilichotokea,” akasema.

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka alilaani tukio hilo akisema ni uvunjaji wa sheria na katiba.

“Kanisa ni eneo takatifu kwa sababu matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia ambaye hajajihami yanaenda kinyume cha katiba,” akasema Bw Musyoka.

“Inasikitisha kuwa watoto, viongozi, akina mama na wale ambao hawajajihami walivamiwa ndani ya kanisa na kurushiwa vitoza machozi na pia risasi kutanda hewani,” akaongeza.

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi aliwataka polisi wawajibishwe kutokana na kitendo hicho.

“Hii si tabia ambayo inastahili kutokea katika nchi inayozingatia demokrasia,” akasema Bw Muturi

Baada ya kutoroshwa, Bw Gachagua alifika nyumbani kwake Wamunyoro na kuwaambia wananchi ambao walikuwa wakimsubiri mjini Othaya waende nyumbani.

Alidai kuwa maisha ya raia yalikuwa hatarini akisema kulikuwa na kikosi hatari cha polisi  kinachoua ambacho kilikuwa kimetumwa eneo hilo na hakujua nia yao.

“Tafadhali fahamu kuwa kuna kikosi  maalum kinachoungwa mkono na polisi na hatujui nina yao baada ya wao kushindwa kuniua ndani ya kanisa,” akaandika Bw Gachagua kupitia mtandao wake wa Facebook.