Habari za Kitaifa

Gachagua: Kikosi cha utekaji nyara kinasimamiwa na Abel, binamu ya afisa wa ngazi za juu serikalini

Na STEPHEN MUNYIRI, MERCY MWENDE December 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amedai serikali ya Rais William Ruto imeunda kikosi maalum cha kuua na kuteka wakosoaji wa serikali.

Bila ufafanuzi wa kina, Bw Gachagua aliendelea kudai kuwa kikosi hicho kinaelekezwa na mtu aliyemtambua kwa jina ‘Abel’ akisema ni binamu wa afisa fulani wa ngazi ya juu serikalini.

Bw Gachagua ameahidi kumwaga mtama kuhusu utambulisho wa wanaohusika na utekaji iwapo maovu haya hayatasitishwa mara moja.

Kulingana na Naibu Rais aliyetimuliwa, kikosi hicho kina makao yake katika jengo moja katikati ya jiji  la Nairobi kwenye ghorofa ya 21.

Bw Gachagua alisema haya alipowahutubia wanahabari nyumbani kwake katika kijiji cha Wamunyoro, Mathira, Kaunti ya Nyeri mnamo Ijumaa.

Alidokeza kuwa utekaji umekithiri na haufai kupuuzwa huku akimtaka Rais Ruto avunje kimya chake kuhusu matukio haya.

“Rais William Ruto anafaa awajibike na aangazie ukiukaji huu kuthibitisha kuwa hahusiki. Kunyamaza kunaashiria matendo haya yanaendelezwa akiwa na ufahamu na kuwa ametoa idhini,” akasema Bw Gachagua.

Wakati huo huo, Bw Gachagua ametaka wakuu wa idara ya usalama wajiuzulu, akiwemo Inspekta Mkuu (IG) wa Polisi Douglas Kanja, Mkurugenzi wa Idara ya Ujajusi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin na Mkurugenzi wa Huduma ya Ujasusi wa Kitaifa (NIS) Noordin Haji akidai ni watepetevu kazini.

“Niliibua masuala kuhusu utekaji wakati wa maandamano ya vijana wa Gen-Z. Nilidhalilishwa niliposema Mkurugenzi wa sasa wa NIS hatoshi. Sasa haya yote yamedhihirishwa waziwazi na ninahisi madai yangu yamethibitishwa,” akaongeza Bw Gachagua.

Idara za usalama zimenawa mikono na kusema hazijajihusisha na utekaji unaoendelea huku shinikizo ikiwa kwa Rais Ruto azungumzie suala hili baada ya kutekwa kwa mchoraji vibonzo Gideon Kibet na kaka yake Rony Kiplangat, Billy Mwangi, Benard Kavuli na ‘Naomi’ ambao walitoweka wakiwa sehemu mbalimbali Embu, Nairobi na Kajiado.

“Nilipozungumza miezi mitano iliyopita nikiwa Mombasa, nilisema tunavunja ahadi tuliyotoa kwa Wakenya ya kutokuwepo tena kwa utekaji na mauaji,” akarejelea kauli kulingana na manifesto ya serikali ya Kenya Kwanza.