Gachagua: Nitatobolea Amerika siri zote za serikali ya Ruto
ALIYEKUWA Naibu Rais wa Kenya, Bw Rigathi Gachagua, amedai kuwa ana habari za ndani kuhusu mikutano ambayo maafisa wa serikali ya Kenya walifanya na viongozi wa makundi ya wanamgambo yanayohusika na migogoro katika eneo la Afrika Mashariki, ikiwemo Sudan.
Bw Gachagua alidai kuwa atawasilisha taarifa alizopata akiwa Naibu Rais kati ya 2022 na 2024 kwa serikali ya Amerika iwapo uchunguzi ambao Seneta mmoja nchini humo anataka Seneti ya Amerika iruhusu Rais Donald Trump kufanya utaanza rasmi.
“Nilikuwa Naibu Rais katika serikali hii wakati mikutano mingi ilifanyika na nina taarifa zote. Nitawapa Waamerika taarifa hizo,” alisema Bw Gachagua wakati wa mkutano uliofanyika Olathe, Kansas City, Amerika, ambako yuko kwa ziara ya miezi miwili.
Bw Gachagua alidai kuwa majibu ya Rais William Ruto kuhusu uchunguzi unaopendekezwa na Amerika unaonuia kuchunguza uhusiano wa Kenya na mahasimu wa nchi hiyo yenye nguvu ulimwenguni, makundi ya wanamgambo na ukiukaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na utekaji nyara.
“Kuna hofu halisi Nairobi. Nilimuona Rais akijaribu kujieleza, lakini aliepuka masuala ya msingi. Alikuwa akisema kuwa Waamerika wana shida naye kwa sababu ana uhusiano na China,” alisema Bw Gachagua.
Aliongeza: “Waamerika wamesikia kilio cha Wakenya na wako tayari kufanya uchunguzi kubaini uovu katika serikali yako ambao unahatarisha amani ya dunia na kukiuka haki za binadamu za Wakenya.”
Ushahidi kuhusu Jenerali Hemedti
Bw Gachagua alisema ana ushahidi kuwa maafisa wa juu serikalini walikutana mara kadhaa na Jenerali Mohamed ‘Hemedti’ Galgalo, kiongozi wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) kinachopigana vita nchini Sudan.
“Amerika haina msimamo wa kuvumilia makundi ya kigaidi, na uhusiano wowote unaoashiria mahusiano na makundi kama hayo unaweza kuathiri hadhi ya Kenya kama mshirika mkuu asiye wa Nato. Hauwezi kukwepa kwa sababu ushahidi upo,” alisema Bw Gachagua.
Mnamo Januari, Idara ya Hazina ya Amerika kupitia Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC), ilitangaza vikwazo dhidi ya Hemedti, ikisema kwa karibu miaka miwili RSF yake iliendesha vita vikali dhidi ya Jeshi la Sudan, kusababisha vifo vya maelfu, kuwahamisha watu milioni 12, na kuchochea njaa kubwa.
Kabla ya kuondolewa madarakani kufuatia kura ya kutokuwa na imani na Bunge mwezi Oktoba mwaka jana, Bw Gachagua alikuwa miongoni mwa waliompokea Hemedti alipowasili JKIA, ingawa baadaye alisisitiza kuwa alifanya hivyo kwa agizo la Rais Ruto.
Bw Gachagua, alisema tayari amekutana na maafisa wakuu wa utawala wa Trump.
Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kigeni ya Seneti ya Amerika, Seneta James Risch, amewasilisha marekebisho ya Mswada unaotaka kupitiwa upya kwa hadhi ya Kenya kama mshirika mkuu asiye wa Nato iliyotolewa Juni 24 2024.
Risch anataka serikali ya Amerika ichunguze madai ya uhusiano wa serikali ya Kenya na makundi ya wanamgambo na magaidi, ikiwemo RSF ya Sudan na Al-Shabaab.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA