Gachagua: Ruto anasuka njama ya kuiba Kalonzo
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amemtaja Rais William Ruto kama kiongozi ambaye ni tishio kwa umoja wa upinzani na sasa anawawinda viongozi wao wakuu wajiunge naye 2027.
Bw Gachagua alidai kuwa Rais Ruto sasa anawatumia baadhi ya wandani wake kumnyemelea kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.
Akizungumza na waumini katika ibada ya kanisa Kasarani, Bw Gachagua alishutumu mbinu hizo akisema zinahujumu demokrasia kwa sababu nia ya rais ni kufanya upinzani uwe dhaifu ndipo ashinde kwa urahisi mnamo 2027.
“Kumekuwa na juhudi kutoka kwa Rais Ruto na wenzake kumshawishi Kalonzo Musyoka ajiunge na mrengo wake. Kuna wengi ambao wanamfuatilia kila mahali ili ajiunge nao,” akasema Bw Gachagua.
Licha ya juhudi hizo alizodai zinaendelezwa na rais, mbunge huyo wa zamani wa Mathira alisema rais hatafaulu kupata uungwaji mkono wa Bw Musyoka na viongozi wengine wa upinzani.
“Nataka niwaambie Wakenya kuwa kama upinzani tunajua kile ambacho kipo akilini mwetu na kwa wakati ufaao tutamteua mwaniaji wa kupambana na William Ruto,” akaongeza Bw Gachagua.
“Uhusiano kati yangu na Kalonzo si kuhusiana na uongozi, siasa au urais bali ni wa kifamilia na ni mzito kuliko maji. Hatutatenganishwa,” akasema Bw Gachagua.
Wakati huo huo, Bw Gachagua alitoa wito kwa uongozi wa ODM kujiondoa kutoka Serikali Jumuishi na kujiunga na upinzani ili kuyaleta mageuzi ambayo Wakenya wanayataka.
Pia upinzani ulisema kuwa utaendesha kampeni kali kuhakikisha kuwa wanashinda viti vingi jijini Nairobi.
Naye Bw Musyoka alitoa wito kwa uwajibikaji na heshima kwa maisha ya Wakenya ambao wanataka mabadiliko.
“Hatutakubali Wakenya wapoteze maisha yao tena jinsi walivyofanya mnamo 2023 na 2024 kwa sababu wana haki ya kushiriki maandamano. Mradi wanafuata sheria, wana haki ya kuandamana,” akasema Bw Musyoka.
Makamu huyo wa rais wa zamani alilalamikia jinsi ambavyo serikali inauza hatimiliki akisema ni njama ya kuwaibia Wakenya.
“Tunataka kusema mashirika ya nchi kama Kampuni ya Mafuta hayafai kuuzwa bila umma kushirikishwa,” akasema Bw Musyoka.
Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya alisema kwamba wakazi wa Nairobi hawajahisi manufaa yoyote katika uongozi wa sasa wa Gavana Johnson Sakaja.
Aliahidi kuwa mabadiliko yatakuja 2027 wakati ambapo upinzani utakuwa usukani mwa siasa za jiji.