Gachagua, ODM waomboleza aliyekuwa mbunge Mathew Lempurkel
ALIYEKUWA Mbunge wa Laikipia Kaskazini, Mathew Lempurkel alifariki dunia jana kutokana na majeraha aliyopata ajalini.
Bw Lempurkel alifariki akipokea matibabu katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), baada ya kuhusika kwenye ajali mbaya ya barabarani mwishoni mwa wiki iliyopita eneo la Rongai, Kaunti ya Kajiado.
Inaripotiwa kuwa Lempurkel alipata majeraha mabaya na kulazwa katika Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU), ambako alifariki dunia.
Kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Bw Rigathi Gachagua, aliongoza kutoa rambirambi akimtaja marehemu kama kiongozi mwaminifu ambaye alijitolea kuhudumia umma.
“Lempurkel alikuwa mwanachama wa DCP na aliwahi kuwa Mbunge wa Laikipia Kaskazini. Roho yake ipumzike kwa amani ya milele, na Mwenyezi Mungu aipe nguvu, faraja na uvumilivu familia yake, wapendwa wake na wote waliompenda wakati huu wa huzuni. Ameondoka, lakini kumbukumbu zake zitadumu daima,” alisema Bw Gachagua.
Bw Lempurkel alihudumu kama Mbunge wa Laikipia Kaskazini kuanzia mwaka wa 2013 hadi 2017 kupitia tiketi ya chama cha ODM.
Alijulikana kwa utetezi wake mkali kuhusu masuala ya jamii ya wafugaji, hasa katika eneo la Laikipia na jamii pana ya Wamaasai.Alipoteza kiti hicho kwa Mbunge wa sasa, Bi Sarah Korere, kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017.
Kupitia taarifa, chama cha ODM pia kilimwomboleza, kikimtaja kama kiongozi mwenye bidii na aliyekuwa na msimamo wa kutetea watu wake.
“Tunamwomboleza Mathew Lempurkel Lekidime, aliyekuwa Mbunge wa Laikipia Kaskazini katika Bunge la 11 kupitia chama cha ODM kati ya 2013 hadi 2017, aliyeaga dunia kufuatia ajali ya barabarani. Amani na faraja ya Mungu iwe juu ya familia yake na watu wa Laikipia wakati huu wa majonzi,” ilisoma taarifa hiyo ya ODM.
Kabla ya kifo chake, Lempurkel alikuwa amehama kutoka chama tawala cha UDA na kujiunga na chama kipya cha DCP.