Gavana Lusaka alivyomkalia ngumu seneta akitaka msamaha kwa kuitwa ‘mpumbavu’
GAVANA wa Kaunti ya Bungoma, Kenneth Lusaka, Jumatatu, Agosti 5, 2024 alisimamisha kwa muda kikao cha Seneti akitaka Seneta aliyemdhalilisha kwa kumtusi kumuomba msamaha.
Bosi huyo wa gatuzi la Bungoma alifika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi ambapo alitakiwa kujibu maswali kuhusu akaunti za Benki ya Commercial (KCB) zinazoendeshwa na kaunti yake.
Hata hivyo, kabla ya kikao hicho kuanza, Gavana Lusaka alieleza Kamati hiyo kwamba Seneta wa Kisii, Richard Onyonka, alimkosea heshima kwa kumwita ‘mpumbavu” na kumtaka aombe radhi.
Haya yalijiri kufuatia ripoti kuwa usimamizi wa kaunti ya Bungoma ulitumia kitita cha Sh25 milioni kwa urembeshaji, ikiwemo kununua maua wakati wa Sikukuu ya Madaraka, mwaka huu, 2024.
Kulingana na Gavana Lusaka, madai hayo hayana msingi wowote kumruhusu Seneta wa Kisii kumshambulia kwa maneno mazito.
“Mialiko hutokana na ripoti ya mdhibiti wa bajeti, ndiposa tuko hapa. Lakini wakati ambapo suala hata halijashughulikiwa na kamati yoyote, mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, mdhibiti bajeti wala EACC, ni uvumi mitaani. Kisha tunalitumia kuunda taswira fulani si haki kabisa ukijua kuwa nitafika hapa,” alisema Gavana Lusaka.
“Mimi ni binadamu na nilihisi nimedhalilishwa kwa kuitwa mpumbavu. Nataka Seneta aombe radhi kwa matamshi hayo.”
Akijitetea, Seneta Onyonka alifafanua kwamba matamshi yake yalitokana na ghadhabu kuhusu ubadhirifu wa fedha uliokithiri Kaunti ya Bungoma akisema hakulenga nafsi ya Gavana.
“Gavana Lusaka wewe ni mwanamme ninayeheshimu mno, hakuna shaka kuhusu hilo. Nilipoona ripoti kuwa Gavana wa Bungoma alinunua maua ya Sh25 milioni nilipandwa na mori. Haikuwa kukuhusu, kauli hiyo haikukulenga. Ikiwa kauli hiyo ilikukwaza ninaomba radhi kwa dhati,” alisema Seneta Onyonka.
“Lakini nitakwambia leo Gavana, nikija leo katika Kituo cha Afya Bungoma nilipokuwa tukiandamana na mwenyekiti, tulipopata wanawake wamelala sakafuni, nakwambia bado nitasema, ‘hawa ni wapumbavu wanaofanya kazi katika kituo kama hiki.’ Mahali tunapowachukulia watu wetu maskini kwa kiwango duni zaidi kuliko tunavyowatendea mbwa wetu.”
Alisema matamshi yake hayakumlenga Gavana Lusaka bali “mifumo mibovu ya taifa langu, Kenya ambapo unasimamia karibu bilioni moja za kufadhili huduma za matibabu na wanawake wote katika kituo hicho…”
“Ukija hapa, huji ili tukueleze jinsi tulivyo safi nawe una hatia. Ni mdahalo jinsi ulivyosema. Uhalisia ni kuwa tulikuwa Bungoma na watu walikuwa wamelala sakafuni tulipoingia. Ukweli ni ule ule ila matamshi, tukizingatia hadhi yako, ninataka kusema samahani kwamba nilikusawiri hivyo.”
Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Wajir, Abass Mohamed, ilielezwa kuwa, Gavana Lusaka vilevile amenukuliwa akitoa matamshi ya kudhalilisha viongozi wengine wakiwemo maseneta.
“Natoka kaunti anayotoka Gavana. Juzi alisema ukiona kobe juu ya meza bila shaka kuna mtu aliyeiwekelea hapo. Lakini sitaichukulia binafsi kwa sababu hatimaye kobe yuko hapa. Tusichukulie mambo kwa kibinafsi,” alisema Seneta Onyonka.