Habari za Kitaifa

Sababu za Gavana Mutai kujitetea mbele ya maseneta wote wiki ijayo

Na COLLINS OMULO August 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Kericho, Dkt Erick Mutai, atafika mbele ya kikao cha wazi cha Seneti wiki ijayo kuanzia Jumatano, Agosti 27 hadi 29, kujibu mashtaka ya kuondolewa mamlakani yaliyopitishwa na Bunge la Kaunti ya Kericho wiki iliyopita.

Hatua hii inafuatia kushindwa kwa Seneti kuunda kamati maalum ya wanachama 11 iliyopendekezwa kuchunguza mashtaka hayo, baada ya hoja ya kuunda kamati hiyo kukosa kufaulu.

Hoja hiyo iliwasilishwa na Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot, lakini Kiongozi wa Wachache, Stewart Madzayo, alikataa kutia saini kuiunga.

Hii ina maana kwamba Seneti sasa itashughulikia suala hilo kupitia kikao cha jumla ambapo maseneta wote 67 watashiriki, lakini ni wale wa kuchaguliwa pekee watakaopiga kura ya mwisho.

Dkt Mutai aliondolewa ofisini mnamo Agosti 15 baada ya madiwani 33 kati ya 47 kupiga kura ya kumuondoa madarakani. Hoja hiyo iliwasilishwa na MCA wa Wadi ya Sigowet, Kiprotich Rogony.

Miongoni mwa tuhuma zinazomkabili ni: matumizi mabaya ya mamlaka, uteuzi wa jamaa wa kifamilia, kuajiri maafisa kinyume cha sheria,kuwafuta kazi maafisa wakuu kiholela, wizi wa rasilmali za umma na malipo ya maradufu kwa wakandarasi.

Vile vile analaumiwa kwas kuvunja sheria za Usimamizi wa Fedha za Umma, Katiba, na Sheria ya Serikali za Kaunti.

Hii ni mara ya pili kwa Dkt Mutai kukumbwa na jaribio la kumng’oa madarakani ndani ya mwaka mmoja.

Mnamo Oktoba 2024, Seneti ilitupilia mbali jaribio la awali baada ya madiwani kushindwa kutimiza kiwango cha thuluthi mbili kinachohitajika kwa mujibu wa Katiba.

Wafuasi wa Gavana Mutai wamezindua kampeni ya kuupinga mchakato huo, wakidai kuwa mfumo wa kura ya kielektroniki uliotumika ulipangwa kabla ili kupotosha matokeo.

Madiwani 18 tayari wametia saini ombi la kupinga mchakato huo na kuwasilisha malalamishi kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).

Katika barua yao kwa DCI, madiwani hao walidai kuwa mfumo wa kura ya mtandaoni haukununuliwa kwa njia halali, haukupitishwa na Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CAK), wala hakukuwa na mafunzo ya awali kabla ya kutumika.

Spika Kingi ameagiza Katibu wa Seneti Jeremiah Nyegenye kutuma mialiko kwa wahusika huku majibu ya pande zote yakitarajiwa kuwasilishwa kufikia Jumatatu, na ratiba ya kesi kusambazwa kwa maseneta Jumanne.