• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Gavana na mbunge wageukia nguvu za Mungu kuhimiza madaktari warejee kazini

Gavana na mbunge wageukia nguvu za Mungu kuhimiza madaktari warejee kazini

NA TITUS OMINDE

GAVANA wa Baringo Benjamin Cheboi na Mbunge wa Ainabkoi, Samuel Chepkonga sasa wanataka nguvu za kiungu kupitia maombi kutumika ili kumaliza mgomo wa madaktari unaoendelea.

Wawili hao walitahadharisha madaktari kuwa Mungu atawaadhibu kwa kwenda kinyume na kiapo chao kutokana na kupenda pesa.

Wakizungumza katika eneobunge la Ainabkoi, Kaunti ya Uasin Gishu wakati wa mazishi ya daktari wa mifugo Peter Kale ambaye hadi kifo chake alikuwa mhadhiri katika chuo cha mafunzo ya ufugaji Naivasha Dairy Training Institute kwa pamoja walionya kuwa Mungu atawaadhibu madaktari kwa kuzingatia zaidi pesa badala ya shida za wagonjwa.

“Nawasihi maaskofu na viongozi wengine wa kidini tuwaombee madaktari wetu Mungu awaguse wajue maisha ya binadamu ni muhimu kuliko fedha na tofauti zao na watu wengine. Pesa haitakupeleka mbinguni hata ukipata kiasi gani, ni hofu ya Mungu pekee ndiyo itakupeleka mbinguni,” alisema Bw Cheboi.

Gavana Cheboi ambaye alipongeza asilimia 70 ya madaktari kutoka kaunti yake kwa kupuuza mgomo na badala yake wanaendelea kuhudumia wagonjwa, alisema kuwa serikali inafanya kila iwezalo kutatua malalamishi yaliyotolewa na madaktari hivyo lazima wazingatie mahangaiko ya Wakenya.

Bw Cheboi alionya madaktari kuwa Mungu atawahukumu vikali kwa kuwaacha wagonjwa wafe huku wakishinikiza nyongeza ya pesa.

Alikumbusha madaktari hatari ya kukiuka kiapo chao cha kulinda maisha huku wakisombwa na tamaa ya pesa nyingi.

“Nashukuru asilimia 70 ya madaktari wangu wanaofanya kazi katika kaunti yangu hawakwenda mgomoni. Wale ambao wanagoma, wajue Mungu atawakuhukumu vikali watakapoenda mbinguni. Mtakuwa na wakati mgumu kueleza Mungu ni kwa nini mlikataa kutibu watu wake wanaolia na kuhitaji matibabu,” akasema Bw Cheboi.

Alisisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kuombea madaktari akimsihi Askofu Stephen Muhando wa kanisa la Toba na Utakatifu aliyekuwa akiongoza shughuli ya maziko kusimamisha shughuli hiyo kwa muda ili kuombea madaktari wote waliogoma ili warudi kazi mara moja.

“Askofu chukua ombi langu kwa uzito hapa tulipo kama nchi tunahitaji maombi kwa ajili ya changamoto hii miongoni mwa mahngaiko tunayokabiliana nayo kama nchi,” akaongeza Bw Cheboi.

Kwa upande wake Bw Chepkonga, aliwashutumu madaktari kwa kukosa utu kwa wagonjwa.

Aliwataka madaktari wanaogoma kuwa na utu kwa wagonjwa akitoa wito kwa kanisa kuomba roho ya Mungu iingie ndani yao ili kuwahurumia wagonjwa wanaoteseka.

“Maaskofu wote waombee madaktari wapokee roho ya Mungu ili waweze kuhurumia wagonjwa wanaoteseka na kurejea kazini ili kutibu wagonjwa wanaopitia mateso mengi kutokana na mgomo,” alisema Bw Chepkonga.

  • Tags

You can share this post!

Uchunguzi: Masomo bora Kenya sasa ni ya matajiri

Watawa walalamikia visa vya wakongwe kutelekezwa jamaa zao...

T L