Gavana wa CBK: Pato la taifa lisipoongezeka itakuwa vigumu kwa Kenya kulipa madeni yake
GAVANA wa Benki Kuu ya Kenya (CBK), Dkt Kamau Thugge, ameonya kuwa nchi inaweza kutatizika kulipa madeni yake ya umma yanayoongezeka, ambayo kwa sasa yamefikia Sh11.8 trilioni, kutokana na changamoto za mtiririko wa fedha katika uchumi.
Dkt Thugge alitoa taarifa hizo mbele ya Kamati ya Madeni ya Umma na Ubinafsishaji ya Bunge, akionyesha kuwa deni linaongezeka kwa kasi zaidi ya Pato la Taifa (GDP).
Mashirika mashuhuri ya kimataifa ya kutathmini mikopo kama Standard & Poor’s (S&P), Fitch Ratings, na Moody’s pia yameeleza hofu kuhusu uwezo wa Kenya kulipa madeni yake kwa wakati.
Mnamo 2023, Kenya ilipewa alama ya mikopo ya B na S&P na Fitch Ratings, huku Moody’s ikitoa kiwango cha B3 na mtazamo hasi. Hata hivyo, Wizara ya Fedha inabainisha kuwa madeni ya umma yapo katika kiwango kinachoweza kudumishwa.
Wachambuzi wa masuala ya fedha katika Ofisi ya Bajeti ya Bunge (PBO) wanafafanua matatizo ya deni kama hali ambapo nchi haiwezi au inapata ugumu kulipa madeni yake, ikimaanisha kuwa haiwezi kulipa riba na madeni makuu kwa wakati.
“Hali hii inaashiria hatari kubwa ya kushindwa kulipa madeni na inahitaji upangaji upya wa deni kwa sababu nchi haiwezi kutimiza ahadi zake za kifedha,” amesema afisa mmoja wa PBO aliyeunganishwa na Bunge.
CBK ina jukumu la kutengeneza na kutekeleza sera ya fedha ya nchi, kutoa sarafu, kusimamia na kudhibiti taasisi za kifedha, na pia kuwa benki ya serikali.
CBK pia inakuza utulivu wa kifedha, kusimamia akiba ya fedha za kigeni, na kusimamia mifumo ya malipo ili kuhakikisha ufanisi na mtiririko wa fedha.
Dkt Thugge alisema madeni ya umma ya Sh11.8 trilioni yaliyoripotiwa katika mwaka wa fedha 2024/25, ni ongezeko la asilimia 11.7 na yalifikia asilimia 69 ya Pato la Taifa Juni 2025.
Mnamo Oktoba 2023, Bunge lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM) kubadilisha kiasi cha juu cha deni la taifa cha Sh10 trilioni kuwa kiwango asilimia 55 ya Pato la Taifa.
Kuongezeka kwa deni, Dkt Thugge alisema, kumechangiwa na mahitaji makubwa ya mikopo na kuongezeka kwa madeni ya ndani na ya nje.
Ili kushughulikia hali hii, Dkt Thugge alisema kuna haja ya kupunguza kasi ya kuongezeka kwa madeni na kupunguza uwiano wa deni dhidi ya Pato la Taifa.
Aliongeza kuwa CBK itaendelea kusaidia utulivu wa uchumi, kuboresha miundombinu ya soko la madeni ya ndani, kuongeza wigo wa wawekezaji na kupunguza hatari ya mabadiliko ya kiwango cha kubadilisha fedha.