Gen Z mtaanza kujiandikisha kuwa wapigakura kuanzia Agosti 2025 – Ethekon
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza kuwa itarejelea mpango wa usajili wa wapiga kura kuanzia Agosti mwaka huu, baada ya shughuli hiyo kusimamishwa kwa miaka miwili.
Mwenyekiti wa tume hiyo Erastus Ethekon Jumamosi alisema shughuli hiyo inalenga kutoa nafasi kwa Wakenya zaidi, haswa vijana waliotimu umri wa miaka 18, kujiandikisha kushiriki katika chaguzi zijazo, kuanzia uchaguzi wa 2027.
“Wakati huu IEBC inakamilisha matayarisho ya ndani na kufikia mwezi ujao wa Agosti, tutatangaza, kupitia gazeti rasmi la serikali, tarehe ambayo tutarejelea usajili wa wapiga kura ili kuwapata Wakenya, waliohitimu, nafasi ya kujiandikisha kuwa wapiga kura,” akawaambia wanahabari mjini Mombasa.
Bw Ethekon alisema tume hiyo haikuweza kuendesha shughuli hiyo mapema kutokana na kutokuwepo kwa mwenyekiti na makamishna wa IEBC.
Kulingana na sheria maamuzi kuhusu suala kama vile usajili wa wapiga kura wapya linapasa kufanywa katika mkutano wa angalau makamishna watatu.
Kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC marehemu Wafula Chebukati, Abdi Guliye na Boya Molu mnamo Januari 17, 2023, tume hiyo ilisalia bila makamishna wa kufanya maamuzi muhimu.
Sababu ni kwamba makamishna wengine wanne; Juliana Cherera (aliyekuwa naibu mwenyekiti), Justus Nyang’aya na Francis Wanderi kulazimishwa kujiuzulu Desemba 20, 2022 kwa kupinga matokeo ya urais yaliyotangazwa na Bw Chebukati mnamo Agosti 15, 2022.
Naye Bi Irene Masit alifutwa kazi Februari 27, 2023 kwa sababu hiyo hiyo kulingana na pendekezo la jopokazi lililoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Aggrey Muchelule.
“Kwa hivyo, bila kuwepo kwetu kama makamishna, sekritariati haingefanya maamamuzi kuhusu suala hili muhimu kwa sababu sheria haiwaruhusu kufanya hivyo,” Bw Ethekon akaeleza.
Mwenyekiti huyo wa IEBC aliongeza kuwa tume hiyo inafahamu kwamba Wakenya wengi wamekuwa wakishinikiza kurejelewa kwa shughuli ya usajili wa wapiga kura. Shinikizo hizo hasa zimekuwa zikitoka kwa vijana na wanasiasa wanaoongozwa na masilahi ya kisiasa.
Bw Ethekon alikubaliana na shinikizo hizo akieleza kuwa ni haki ya kila Mkenya kushiriki katika shughuli za kidemokrasia.
“Miito hii haswa inatoka kwa kizazi cha vijana ambacho kina hamu ya kushiriki katika michakato ya kidemokrasia, haswa uchaguzi wa 2027, kulingana na hitaji la Katiba.
Bw Ethekon alikariri umuhimu wa kuundwa kwa sajili sahihi na jumuishi ya wapiga kura, akiitaka kama msingi wa uendeshaji wa chaguzi huru, haki na yenye uwazi.
“Uaminifu wa uchaguzi wowote unategemea usahihi na ubora wa sajili ya wapiga kura. Hii sio kwa ajili ya masuala ya kiusimamizi bali ni kuwezesha kuwekwa kwa misingi chaguzi huru, haki na yenye uwazi,” akaeleza.
Bw Ethekon pia alikariri kuwa IEBC itaendelea kufanya mazungumzo na wadau inapotekeleza majukumu yake.
Mwenyekiti huyo na makamishna sita wamekuwa Mombasa tangu Alhamisi wiki jana kwa shughuli ya uhamasisho kuhusu majukumu yao.
Katika uchaguzi mkuu wa 2022, sajili ya wapiga kura ilikuwa na jumla ya wapiga kura 22 milioni.
Sasa IEBC ikadiria kwamba itaweza kuongeza angalau wapiga kuwa 14 milioni katika idadi hiyo kwa ajili uchaguzi mkuu wa 2027.