Habari za Kitaifa

Gen Z wa Indonesia wachoma mabunge maandamano yakichacha

Na REUTERS, BENSON MATHEKA August 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

JAKARTA, Indonesia,

RAIS wa Indonesia, Prabowo Subianto, siku ya Jumamosi alifuta safari yake iliyopangwa kwenda China baada ya maandamano yaliyoanza jijini Jakarta kuenea hadi maeneo mengine, huku baadhi ya majengo ya mabunge ya mikoa yakichomwa moto.

Prabowo alitarajiwa kuhudhuria gwaride la “Siku ya Ushindi” nchini China Septemba 3, kuadhimisha miaka 80 tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia baada ya Japan kujisalimisha rasmi.

Maandamano hayo, ambayo ni mtihani mkubwa wa kwanza kwa serikali ya Prabowo iliyotimiza karibu mwaka mmoja madarakani, yalianza wiki hii Jakarta kufuatia malalamishi kuhusu mishahara ya wabunge na yakazidi baada ya gari la polisi kumgonga na kumuua mwendesha pikipiki.

“Rais anataka kuendelea kufuatilia hali nchini moja kwa moja… na kutafuta suluhisho bora,” msemaji wa rais, Prasetyo Hadi, alisema kupitia taarifa ya video siku ya Jumamosi.

“Kwa hivyo, rais anaomba radhi kwa serikali ya China kwa kushindwa kuhudhuria mwaliko huo.”

Prasetyo aliongeza kuwa sababu nyingine ya kufuta safari hiyo ni kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachotarajiwa kufanyika Septemba.

Kufuatia maandamano hayo, kampuni ya TikTok, inayomilikiwa na ByteDance ya China, ilitangaza Jumamosi kuwa imesitisha huduma yake ya matangazo ya moja kwa moja kwa muda wa siku chache nchini Indonesia.

Serikali ya Jakarta wiki hii iliita wawakilishi wa majukwaa ya mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na Meta Platforms Inc na TikTok, na kuwataka kuongeza juhudi za kudhibiti maudhui kutokana na kusambaa kwa taarifa potofu mitandaoni. Serikali inasema taarifa hizo za uongo zimechochea maandamano dhidi yake.