Gen Z waombwa kusitisha maandamano
VIONGOZI wa kidini, wakiongozwa na Baraza la Maimamu na Wahubiri Nchini (CIPK) wamewataka vijana nchini Kenya kusitisha maandamano yao yanayotarajiwa kuendelea kesho, Jumanne, Julai 16, 2024 wakihofia kudorora kwa usalama.
Wakiongozwa na Katibu Mwenezi Sheikh Mohammed Khalifa, wanasema maandamano hayo yameonyesha uzito wa kuvuruga amani ya nchi, ikiwemo kusababisha maafa na uharibifu wa mali.
CIPK inasema licha ya kuwa maandamano ni haki ya Kikatiba, wanaoshiriki wanapaswa kuwa waangalifu kuhakikisha amani inadumishwa.
Waliwataka vijana kupeana nafasi ya mazungumzo ili maelewano yawepo.
“Ili kuepuka maafa, tunaomba vijana wetu wasiandamane. Wanapokwenda barabarani kila mzazi roho yake inakuwa mkononi, presha juu, sukari inapanda watu hawalali wakisubiri kuona ikiwa watarudi nyumbani salama, viwete ama maiti,” alisema Sheikh Khalifa.
Alisema wakora wamevamia maandamano hayo na kuanza kutishia usalama.
Kiongozi huyo wa kidini alisikitikia maandamano hayo kuleta madhara hasa kwa wafanyibiashara.
Mwekahazina wa kitaifa, Sheikh Hassan Omar alisema yameleta madhara kwa Wakenya, uharibifu wa mali na kusababisha vifo.
“Tunataka amani idumu katika taifa letu la Kenya, wito wetu kwa vijana ni waache kuvuruga nchi yetu. Nchi ikiharibika hakuna atakayesazwa. Tupeane nafasi kwa mazungumzo,” alisema Sheikh Omar.