Habari za Kitaifa

Gideon akanusha kujiondoa kwake Baringo ni kwa ajili ya kulinda biashara

Na MOSES NYAMORI, JUSTUS OCHIENG October 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MWENYEKITI wa chama cha Kanu, Gideon Moi, jana alijiondoa katika kinyang’anyiro cha useneta wa Baringo, na kumuacha mgombeaji wa chama cha UDA, Vincent Chemitei pazuri kutwaa ushindi.

Bw Moi alifanya uamuzi huo saa chache baada ya kukutana na Rais William Ruto ambaye ni kiongozi wa UDA.

Wadokezi kadhaa waliambia Taifa Leo kuwa uamuzi huo wa ghafla ulitokana na “masuala ya kibiashara”.

Familia ya rais wa zamani Daniel arap Moi imewahi kulalamika wazi kwamba serikali ya Kenya Kwanza imekuwa ikitumia Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) kama silaha dhidi yake.

Jana, barabara zote zilielekea Kabarnet huku wafuasi wa Kanu waliovalia mavazi ya rangi nyekundu wakicheza, kuimba na kupeperusha bendera nje ya afisi za tume ya uchaguzi ya IEBC wakimsubiri Moi kuwasilisha karatasi zake za uteuzi kwa uchaguzi mdogo wa useneta Baringo.

Ilipofika saa tano asubuhi, matarajio yaligeuka kuwa wasiwasi.

Habari zilianza kusambaa kwamba ‘Mwenyekiti’, kama anavyojulikana, alikuwa njiani. Kufikia saa nane mchana, minong’ono ya hofu ilianza kusikika.

Na ilipofika saa kumi jioni, muda wa mwisho wa IEBC kupokea karatasi za uteuzi, ikawa wazi Gideon Moi hangefika.

Hatimaye, ilibainika kuwa mwana wa rais wa pili wa Kenya alikuwa amejiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Mabadiliko haya yalijiri siku moja tu baada ya Moi kutembelea Ikulu ya Nairobi ghafla, alipokutana na Rais Ruto akiwa na Katibu Mkuu wa Kanu, George Wainaina, na aliyekuwa Mwakilishi wa Kike wa Baringo, Gladwel Cheruiyot.

Jana jioni, Bw Wainaina alithibitisha kuwa Moi hatawasilisha karatasi zake kwa tume, akitaja “masuala mengine” kuwa sababu ya kujiondoa.

“Hatutawasilisha karatasi za uteuzi kwa sababu kuna masuala mengine yanayoangaziwa,” Wainaina aliambia Taifa Leo.

Alipoulizwa ikiwa masuala hayo ni ya kibiashara, alijibu.

“Si ya kibiashara. Tulikubaliana kama vyama. Kuna pendekezo lililotufikia na tukakubaliana. Tulifanya mashauriano zaidi na tukakubali kujiondoa.”

Alikanusha madai kuwa Kanu imefanya makubaliano ya kisiasa na Ruto kama yale ya ODM-UDA.

“Huyo ni rais wa nchi. Akituita kwa kikao kujadili masuala muhimu, tunaenda. Sisi ni chama cha kitaifa na kuhudhuria mkutano hakumaanishi tumejiunga na serikali,” alisema.

Hata hivyo, duru zilieleza kuwa Moi alikubali kujiondoa katika uchaguzi huo ili kulinda biashara za familia yake, ambazo zimekuwa zikikumbwa na changamoto kubwa chini ya utawala wa Rais Ruto.

Baadhi ya biashara zake zimekuwa na matatizo na KRA kuhusu madeni ya ushuru, huku baadhi ya kampuni zikipokonywa leseni hivi majuzi.

Familia ya Moi ina uwekezaji mkubwa katika sekta ya kawi na madini.

Afisa mmoja wa Ikulu alidokeza kuwa Moi aliomba serikali iingilie kati ili biashara zake ziweze kurudi katika hali ya kupata faida.

“Maombi yake yalihusiana na biashara zake. Unajua biashara zake zimekuwa zikisuasua kwa miaka mitatu iliyopita,” alisema.

Mapema mwaka huu, kampuni ya uzalishaji umeme inayomilikiwa na familia ya Moi ilipata pigo baada ya mahakama ya Nakuru kufuta leseni ya kufanya utafiti wa nishati katika mradi wa Geothermal Development Company eneo la Menengai.

Jaji Milicent Odeny wa Mahakama Kuu alifuta Ripoti ya Tathmini ya Athari za Mazingira (EIA) iliyotolewa kwa kampuni ya Sosian Energy Ltd na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA).

Sosian Energy, kampuni ya familia ya Rais Daniel arap Moi, ndiyo ya pekee inayochimba visima katika mashamba ya kawi ya mvuke ya Menengai.

Kigen Moi, mtoto wa Gideon, ni mkurugenzi wa kampuni hii.

Baadhi ya viongozi wa Kanu, ambao Jumatano walisema kuwa Moi alipinga takwa la Rais kuwa ajiondoe katika uchaguzi mdogo kumwachia Chemitei, jana walisema walitamaushwa na uamuzi huo.

Walisema Moi alizima simu yake na kwamba alitumia uaminifu na msaada wa wanachama wa Kanu kwa manufaa yake binafsi.

“Alipaswa kuwaandaa wafuasi wake ili wahisi kuheshimiwa. Njia aliyochagua kujiondoa haikuwa nzuri. Inazua mvutano ndani ya chama,” alisema mmoja wa viongozi.

Mnamo Oktoba 2, Kanu ilitangaza uteuzi wa Moi, ikisema ulifanywa baada ya mashauriano ya kina ndani ya chama na watu wa Baringo.

Wachambuzi wa siasa wanasema kujiondoa kwa Moi kunaweza kuleta athari kubwa kisiasa. Kwa Ruto, inampa udhibiti wa ngome yake ya nyumbani kwa kuepusha mgombea wa UDA kushindwa.

Chini ya utawala wa Rais Ruto, Kanu imepoteza ushawishi pakubwa, katika eneo la Rift Valley ambalo wakati mmoja ilikuwa na wabunge wengi hadi kubaki na kimoja.

Kwa sasa kimebaki na kiti cha eneobunge la Tiaty linalowakilishwa na William Kamket.