Habari za Kitaifa

Gumo, Khaniri watilia shaka namna Jirongo alivyofia ajalini

Na STEVE OTIENO December 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI wa zamani Fred Gumo na aliyekuwa Seneta wa Vihiga George Khaniri wametaka uchunguzi ufanywe kuhusiana na kifo cha Mbunge wa zamani Cyrus Jirongo.

Wawili hao walishangaa jinsi ambavyo mbunge huyo wa zamani wa Lugari alivyosafiri kutoka Karen hadi Naivasha ilhali alikuwa akienda nyumbani kwake Gigiri Ijumaa usiku.

Bw Khaniri alisema Naivasha ni mbali na wanataka kujua jinsi ambavyo Bw Jirongo alivyofika huko kisha akapata ajali akitokea Naivasha kuja Nairobi.

Wakati wa mauti hayo ya kuamkia Jumamosi, Bw Jirongo alikuwa pekee kwenye gari lake ambalo liligongana na basi la Climax akitoka kituo cha mafuta Naivasha.

Basi la Climax lilikuwa limetoka Nairobi.

Bw Gumo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya mazishi ya mwendazake alisema kuna kamera maeneo mbalimbali jijini na polisi wanastahili kuziangalia katika juhudi za kufahamu ukweli.

“Hakuwa anaenda nyumbani kwake Kakamega, alikuwa asafiri kutoka Karen hadi kwake Gigiri. Inakuaje sasa alikuwa akisafiri tena kutoka Naivasha hadi Nairobi? Kuna kamera kote kote na wakiangalia watafahamu ukweli,” akasema Bw Gumo.

Kamati andalizi ya mazishi imesema kuwa Bw Jirongo atazikwa Lugari mnamo Desemba 30, 2025.

Mwili wake utapelekwa nyumbani kwake Gigiri mnamo Desemba 27 kisha usafirishe Kitale kwa mke wake wa pili Desemba 28.

Siku inayofuata ya Desemba 29 utapelekwa nyumbani kwake Lumakanda, Lugari kisha mazishi yafanyike Desemba 30.