Hafla 2 muhimu alizopanga Raila kabla ya kufariki
WAFUASI wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, wanasikitika kwamba kifo chake kimetokea kabla ya kushiriki matukio mawili muhimu ambayo yalikuwa ya dhati moyoni mwake – sherehe za kutimiza miaka 20 ya chama cha ODM, na kongamano la kimataifa la uwekezaji katika Kaunti ya Siaya.
Kwa wengi walioamini katika uongozi wa Bw Odinga, uwepo wake katika maadhimisho ya miaka 20 ya chama alichokiasisi baada ya kura ya maamuzi ya mwaka 2005, ungedhihirisha heshima kwa wafuasi wake kote nchini.
Chama cha ODM kilikuwa kimepanga sherehe hiyo kuanzia Oktoba 10 hadi 12 jijini Mombasa, lakini iliahirishwa hadi Novemba 14-16, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa kamati ya maandalizi, Junet Mohamed.
Taarifa hiyo ilisema kuwa uamuzi huo ulifikiwa baada ya mashauriano ya kina na viongozi wakuu wa chama, kwa lengo la kuhakikisha kwamba hafla hiyo ni jumuishi kwa maeneo yote.
Bw Odinga alisisitiza kuwa bado kuna kaunti ambazo hazikushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo, na kwamba kuendelea na sherehe za Mombasa kabla ya maeneo hayo kungepunguza uzito wa mchango wa wafuasi katika maeneo mengine.
Tayari ODM ilikuwa imefanya maadhimisho hayo katika Busia, Wajir, Kisii na Narok.
Hata hivyo, wakati wa sherehe katika uwanja wa Gusii mwezi Septemba, Bw Odinga hakufika.
Wapo waliodai kuwa afya yake ilikuwa imedorora, na alihitaji muda wa kupona kabla ya kushiriki hafla kubwa ya Mombasa.
Sasa, haijulikani iwapo sherehe hizo zitaendelea kama zilivyopangwa mwezi ujao, hasa baada ya kifo chake.
Katika taarifa ya Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, chama hicho kiliahidi kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mipango ya mazishi kwa ushirikiano na familia, lakini hakikusema lolote kuhusu hatima ya maadhimisho ya ODM@20.
“Tunapoendelea kushughulikia habari hizi za kusikitisha, na kusubiri taarifa zaidi, nawasihi wanachama wote wa chama kudumisha mshikamano na umoja huku tukitafakari maisha na mchango wa kiongozi wetu – mtu aliyekuwa mfano na baba kwa wengi, ‘Baba’,” alisema Bw Sifuna.
Kwa bahati mbaya, Raila hatapata fursa ya kusherehekea historia ya chama kilichoibuka kutoka kwa kampeni ya kupinga katiba ya 2005, ambapo alama ya chungwa iliwakilisha upande wa “Hapana”, ulioshinda kwa asilimia 58.