Habari za Kitaifa

Hafla ya kumuomboleza Aga Khan kufanyika leo Ureno

Na  DANIEL OGETTA February 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HAFLA ya mazishi ya Mwadhama Mwanamfalme Karim Al-Hussaini Aga Khan IV itafanyika leo katika Kituo cha Ismaili huko Lisbon, Ureno.

Hafla hiyo itahudhuriwa na wageni walioalikwa pekee, wakiwemo watu wa familia ya Aga Khan, viongozi wa jamii ya kimataifa ya Ismailia na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan, watu mashuhuri wa kimataifa na maafisa wa serikali ya Ureno.

Hafla hiyo itaonyeshwa moja kwa moja na The Ismaili TV, kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa Alhamisi.

Aga Khan IV, Imam wa 49 wa Waislamu wa Shia Ismaili, atazikwa katika sherehe ya faragha huko Aswan, Misri, Jumapili.Wakati huo huo, sherehe za kumtawaza rasmi kiongozi mpya wa kiroho wa Waislamu wa Shia Ismailia Mwanamfalme Rahim al-Hussaini Aga Khan V, zitafanyika mjini Lisbon siku ya Jumanne.

Aga Khan V atawapa nafasi viongozi wakuu wa Ismailia ambao watatoa kiapo cha utiifu wao kwa niaba ya jamii ya kimataifa ya Ismailia, kwa Imamu wa 50 katika hafla ya faragha ya kidini.

Akiongea Alhamisi baada ya kutia saini kitabu cha rambirambi katika afisi za Baraza la Ismaili nchini Kenya, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, alimtaja Mwadhama Aga Khan IV, kama kiongozi mkarimu ambaye miradi yake ya kusaidia jamii imeenea kote ulimwenguni ikiwemo maeneo yenye changamoto kama vile Afghanistan.

“Nachukua fursa hii kumtakia heri njema kiongozi mpya, wa 50, Mwanamfalme Rahim, anayechukua usukani. Tunampa baraka zetu anapochukua uongozi. Muhimu zaidi tunamwombea baraka za Mungu,” akasema Bw Mudavadi.

Mwadhama Mwanamfalme Karim Al-Hussaini Aga Khan IV, kiongozi wa 49 wa dhehebu la Waislamu la Shia Ismaili, alikuwa mwanzilishi na mwenyekiti wa Shirika la Maendeleo la Aga Khan (AKDN).Alikufa Jumanne jijini Lisbon, Ureno, akiwa na umri wa miaka 88, akiwa amezingirwa na watu wa familia yake.

Nchini Kenya, sawa na maeneo mengine ya ulimwenguni, shirika la AKDN limefanya kazi katika sekta nyingi zikiwemo elimu, afya na zingine za kiuchumi.Limechangia pakubwa katika kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari kupitia Shirika la Habari la Nation (NMG).Michango hii, Bw Mudavadi alisema, “imebadilisha maisha ya watu wengi, na taasisi zake zitaendelea kufanya hivyo, huku zikiendeleza na kukuza kumbukumbu yake.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA