Habari za Kitaifa

Hakimu adinda kuamuru mshukiwa wa wizi wa Sh1.5 bilioni afikishwe kortini

Na RICHARD MUNGUTI August 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HAKIMU Mwandamizi Geoffrey Onsarigo ametupilia mbali ombi linalotaka polisi wamfikishe mahakamani meneja wa benki ya Equity anayezuiliwa kwa tuhuma za wizi wa Sh1.5bilioni mwezi uliopita.

Huku Onsarigo akitupilia mbali ombi la kushurutisha polisi wamshtaki David Machiri Kimani, familia yake iko hoi taabani kwa hofu kwa sababu ‘hawajui anakozuiliwa na polisi kwa vile jitihada za kumfikia zimegonga ukuta.’

Mawakili Njiru Ndegwa, Dkt Paul Macira Gitau, Alex Gakuru na Harun Ndubi waliambia korti Ijumaa kwamba polisi wamekuwa wakimhamisha Machiri kutoka kituo kimoja cha polisi hadi kingine.

“Mara ya mwisho tulipowasiliana na Machiri alikuwa amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Capitol lakini sasa ameondolewa hapo. Hatujui alikopelekwa,” mawakili hao walilalamikia mahakama.

Ndegwa alilalamikia mahakama kwamba polisi wamekuwa wakiwachezea kila mmoja.

“Polisi walikuwa wamfikishe Machiri kortini lakini hawakumlete kama ilivyoamriwa na hii mahakama. Wamekaidi agizo la hii korti. Wameidharau hii mahakama,” Bw Ndegwa aliambia hakimu Ijumaa kwa ghadhabu.

Mawakili hao wanne walilumbana na kiongozi wa mashtaka aliyeeleza mahakama kwamba “hajapokea taarifa yoyote kuhusu aliko mshukiwa huyo.”

Lakini Mabw Ndegwa, Gitau, Ndubi na Gakuru walidumisha msimamo wao kwamba lazima mteja wao afikishwe kortini  ashtakiwe ama aachiliwe.

Mawakili hao walieleza mahakama iwapo mshukiwa huyo hatafikishwa kortini basi itabidi Inspekta Jenerali wa polisi aagizwe afike kortini aeleze aliko David Machiri Kimani aliyetiwa nguvuni Agosti 4,2024 na kuzuiliwa.

Mahakama ilielezwa mshukiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 na kuagizwa awe akiwasiliana na afisa anayechunguza kesi hiyo mara mbili kwa wiki.

Lakini Inspekta Bonface Mwangi wa kitengo cha ufisadi katika Benki Kuu ya Kenya (CBK) alieleza mahakama Machiri alifika katika afisi yake mara mbili kisha akachana mbuga.

Ijapokuwa mawakili waliomba Machiri afikishwe kortini, Onsarigo alisema hana uwezo kisheria kuagiza polisi wamsalamishe mara moja mshukiwa huyo kortini.

Onsarigo alisema jukumu hilo ni la mahakama kuu na akawashauri mawakili Ndegwa na wenzake waelekee mahakama kuu kuomba haki za mshukiwa zizingatiwe.

Mawakili hao walizubaa kortini huku wasijue la kufanya.

Machiri anashukiwa kuiba Sh1,545,887140.49 kutoka kwa benki hiyo.