Hakimu akimbizwa hospitali baada ya kupigwa risasi na polisi kortini
NA FATUMA BARIKI
HAKIMU katika Mahakama ya Makadara, Nairobi anauguzisha jeraha la risasi, baada ya kushambuliwa na afisa wa polisi wakati kesi ikiendelea kortini Alhamisi alasiri.
Kulingana na taarifa kutoka kwa Msajili Mkuu wa Mahakama Winfridah Mokaya, hakimu huyo aliyetambuliwa kama Monicah Kivuti alikuwa anasikiza kesi ambapo mshukiwa alikiuka masharti ya dhamana, hivyo hakimu akafutilia mbali dhama hiyo baada ya kukosa kuridhika na maelezo yaliyotolewa na mshukiwa.
“Punde tu hakimu alipotoa uamuzi huo, mtu fulani alimpiga risasi na kumjeruhi kwenye nyonga. Maafisa wa polisi waliokuwemo walimkabili aliyepiga risasi na kummaliza, huku hakimu akikimbizwa hospitali,” ikasema taarifa hiyo.
Ilibainika baadaye kwamba mpigaji risasi alikuwa afisa wa polisi ambaye ni mume wa mshukiwa ambaye kesi yake ilikuwa inasikizwa.
“Tungependa kuhakikishia maafisa wote wa mahakama kwamba usalama wao umedhibitiwa. Kuendelea mbele, tutaangalia upya mikakati ya kiusalama kuhusu wote wanaohudhuria vikao kortini, pamoja na maafisa wa polisi wanaozuru mahakama wakati ambapo hawahitajiki kubeba silaha,” akasema Bi Mokaya.