Habari za Kitaifa

Hakuna aliye salama, viongozi wasema baada ya Jaji Koome kupokonywa walinzi

Na WINNIE ONYANDO January 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS wa Bunge la Mwananchi Francis Awino amekemea hatua ya serikali ya kumpokonya Jaji Mkuu Martha Koome walinzi.

Akizungumza na Taifa Dijitali Januari 24, 2025, Bw Awino alisema hatua hiyo inaonyesha kuwa hakuna aliye salama nchini.

“Ikiwa Jaji Mkuu analilia haki, je, mwananchi wa kawaida atafanya nini? Hili ni jambo linalofaa kuangaziwa kwa undani na hatua ya haraka kuchukuliwa,” akaema Bw Awino.

Kando na hayo, alisema kuwa kumpokonya Bi Koome walinzi kunaonyesha mgawanyiko mkubwa katika serikali.

“Hii inaonyesha kuwa kuna mzozo kati ya serikali ya Kenya Kwanza na mahakama.”

Hatua ya kumpokonya Bi Koome walinzi imezua mjadala nchini huku baadhi ya viongozi wakilaani hatua hiyo.

Chama cha wanasheria nchini (LSK) kikiongozwa na rais wao Faith Odhiambo pia kimelaani hatua hiyo kikisema kuwa inakiuka uhuru wa mahakama.

Bi Odhiambo alisema uamuzi wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi pia unaangazia juhudi zilizoratibiwa za kudhoofisha Kitengo cha Polisi cha Mahakama.

“Hatua hiyo haikubaliki na inaonyesha upungufu mkubwa wa kimfumo na kiutawala ndani ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi,” alisema Bi Odhiambo.

Bi Koome, katika barua aliyowaandikia Waziri wa Ulinzi wa Ndani Kipchumba Murkomen na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, alidai kuwa alipokonywa walinzi wake na hata idadi ya maafisa waliotumwa kortini chini ya Kitengo cha Polisi cha Mahakama ilipunguzwa.

Japo Bi Koome hakutaja idadi kamili ya maafisa walioondolewa, Chama cha Mahakimu na Majaji nchini kilidai kuwa maafisa 23 chini ya Kitengo cha Polisi cha Mahakama wameathirika.

Akijitetea Ijumaa, Januari 24, 2025, Bw Murkomen alimhakikishia Jaji Koome usalama wake, akisema ni maafisa watatu tu kati ya 29 wa usalama walioondolewa.

“Maafisa wanapopandishwa vyeo, ​​wanahitaji kupata mafunzo. Kwa bahati mbaya, Jaji Mkuu alijitokeza hadharani kuhusu suala hili. Hata hivyo, namhakikishia kuwa suala hilo litatatuliwa,” alisema.

Alizungumza akiwa katika uzinduzi wa Kitengo cha Polisi cha Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAP) ambapo alimlaumu Bi Koome kwa ‘kuanika suala hilo hadharani.’

Pia, alifafanua kuwa maafisa hao wa usalama walipandishwa vyeo na walikuwa wameenda kupokea mafunzo.