Hakuna muda wa kutengeneza mipaka mipya; kura ifanyike kwanza -IEBC
WAKENYA wataenda uchaguzi mkuu wa 2027 wakitumia wadi na maeneobunge ya sasa baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) kusema hakutakuwa na mipaka mipya.
IEBC Jumanne ilitangaza kuwa itafanyia marekebisho mipaka mipya ya wadi na maeneobunge baada ya uchaguzi mkuu wa 2027, ikisema kwa sasa shughuli hiyo haiwezekani kabla ya kura kupigwa mwakani.
Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon mnamo Jumanne alisema uamuzi huo umetokana na muda uliosalia kabla ya uchaguzi mkuu ujao, kesi zilizoko mahakamani kuhusiana na takwimu za sensa ya 2019 na kuvurugika kwa ratiba ya uchaguzi mkuu ujao.
“Kutokana na vikwazo vya kisheria, kesi na uchaguzi mkuu wa 2027 kukaribia, tume imeamua kuwa hakutakuwa na mipaka mipya ya maeneobunge na wadi kabla ya uchaguzi huo kuandaliwa,” akasema Bw Ethekon.
“Mipaka mipya ya maeneobunge na wadi itaangaziwa baada ya uchaguzi mkuu wa 2027 kwa kutumia data ambayo haijawekewa vikwazo kisheria na haina utata,” akaongeza.
Kwa sababu uchaguzi mkuu ujao umekaribia, IEBC sasa itamakinikia masuala yanayoambatana na kura hiyo miezi 12 kabla ya kuandaliwa kwake.
Hasa itamakinikia usajili wa wapigakura, chaguzi ndogo na maandalizi mengine ya uchaguzi mkuu.
Sasa ni dhahiri kuwa mabadiliko kwenye mipaka itafanyika kabla ya 2032 lakini Wakenya wataendea debeni mwaka ujao kwa kutumia maeneobunge 290 pamoja na wadi 1,450 za sasa.
Kwa mujibu wa katiba, kuangazia upya kwa mpaka wa eneobunge au wadi huchukua zaidi ya miaka miwili na katiba hiyo hiyo inasema mabadiliko hayo yanastahili kukamilika miezi 12 kabla ya kura kupigwa.
Aidha, Katiba yenyewe inaamrisha IEBC iangazie upya mipaka yake baada ya kati ya miaka minane hadi 12.
Mara ya mwisho IEBC iliangazia mipaka ya maeneobunge ni Machi 2012 na baada ya miaka 12, mipaka mipya ilistahili kuangaziwa Machi 2024.
Makataa yalipita bila mipaka mipya kuangaziwa kwa sababu IEBC haikuwa na makamishina na pia kuna kesi kortini.