Habari za Kitaifa

Hali si shwari kwa mawaziri wa Raila serikalini kufuatia tamko lake kuhusu 2027

Na JUSTUS OCHIENG’ September 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KAULI ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga wiki iliyopita kuashiria chama chake kitakuwa na mgombeaji wa urais mwaka wa 2027 imezua tumbojoto kwa washirika wake walio serikalini.

Kauli hiyo ilitikisa siasa za kitaifa na kuibua suitafahamu si kwa upande wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais William Ruto tu, ambao umekuwa ukitegemea usaidizi wa Raila katika uchaguzi ujao, bali pia kwa wandani wake walio serikalini kupitia mkataba wa ushirikiano kati ya ODM na UDA.

“Nani aliwaambia kwamba ODM haitakuwa na mgombeaji wa urais 2027? Kwanza, fikirieni kama ODM. Tuna mpango wa wazi ambao tumejadiliana na kukubaliana. Maamuzi mengine yatazingatiwa wakati ufaao,” Raila alisema kwenye mkutano huo wa Jumatatu.

Kauli hiyo ilijiri wiki chache tu baada ya Raila kuwahakikishia waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Karachuonyo Phoebe Asiyo kuwa mpango wa Serikali Jumuishi kati yake na Rais Ruto utaendelea hadi 2027.

Hali hiyo iliwatia moyo viongozi wa ODM waliojiunga na serikali na kuteuliwa katika nyadhifa mbalimbali za uwaziri na mashirika ya serikali.

Hata hivyo, baada ya kauli yake mpya, baadhi ya wafuasi wake walio serikalini wanaripotiwa kuwa na hofu kuhusu ikiwa kiongozi huyo yuko tayari kusambaratisha ushirikiano wao na Rais Ruto au la.

Katika miezi ya hivi karibuni, Rais Ruto ameendeleza juhudi za kuwanasa wandani wa karibu wa Raila katika serikali yake.

Kutoka kwa nyadhifa za uwaziri kama Opiyo Wandayi (Kawi), John Mbadi (Wizara ya Fedha), Hassan Joho (Madini), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika), na Beatrice Askul (EAC), hadi uteuzi wa marafiki wa Raila katika mashirika ya serikali, orodha ya wanachama wa ODM serikalini inazidi kuongezeka.

Hivi majuzi, Rais alimteua Prof Lawrence Gumbe, mshirika wa zamani wa Raila tangu enzi za NDP na LDP, kuwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Kawi ya Nyuklia.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Maji ilimfuta kazi Odoyo Owidi ambaye ni mpinzani wa Raila, na kumteua Daniel Shem Omino, mtoto wa marehemu Joel Omino, aliyekuwa mshirika mwaminifu wa Raila.

Mawaziri kutoka upande wa ODM pia wamekuwa wakiteua washirika wao katika bodi za mashirika ya serikali.

Waziri Wandayi alimteua Anne Michura katika Mamlaka ya Kawi ya Nyuklia, huku George Odhiambo Oballa akipata nafasi katika Kituo cha Rasilmali za Vinasaba vya Mifugo.

Wachambuzi wanasema kuwa hatua hizi ni sehemu ya mkakati wa Rais Ruto kuhakikisha anaungwa mkono na Raila ama angalau asipingwe vikali mwaka wa 2027.

Makubaliano ya ODM-UDA yaliyotiwa saini mwezi Machi mwaka huu yanaangazia vipengele 10 vikiwemo ushirikishaji, ugatuzi, vita dhidi ya ufisadi, ukaguzi wa deni la umma, uwezeshaji wa vijana, na utetezi wa haki za binadamu.

Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga ambaye ni kaka yake Raila, alisema ikiwa makubaliano hayo yatekelezwa ipasavyo, basi ODM inaweza kumuunga mkono Rais Ruto mwaka wa 2027.

“Makubaliano yetu na serikali yanalenga ajenda 10 tunazotaka kufanikisha kupitia ushirikiano. Tutashirikiana nao hadi 2027, na tukiridhika kuwa tumehudumiwa vyema, tutaendelea. La sivyo, tutatengana,” alisema Dkt Oginga.

Lakini kauli mpya ya Raila imeacha hata wafuasi wake wa karibu wakibahatisha hatua atakayochukua.

“Muda mwingine, kuhudumia taifa ni muhimu zaidi kuliko siasa za vyama,” mmoja wa walioteuliwa kutoka upande wa Raila aliambia Taifa Leo, akionyesha uwezekano wa kumkaidi kiongozi huyo iwapo ataamua kujiondoa kwenye ushirikiano huo wa kisiasa.

Mwingine alisema: “Nimekuwa mwaminifu kwa Raila, lakini nyakati hubadilika. Hatuwezi kuendelea kuishi katika suitafahamu ya kisiasa. Si lazima tumfuate tena kwenye kinyang’anyiro kingine.

“Wengine wetu tumejijengea nafasi serikalini na tunataka kuhudumu. Siwezi kujiuzulu kwa sababu ya mabadiliko ya kisiasa. Uaminifu wangu ni kwa nchi.”

Rais Ruto, ambaye pia anakabiliwa na changamoto kutoka kwa baadhi ya washirika wake wa karibu kama vile aliyekuwa Naibu wake Rigathi Gachagua ambaye ameanzisha chama kipya, hawezi kufungua nafasi ya kupoteza kisiasa.

Kwa Rais, msimamo wa Raila unaweza kuleta tofauti kati ya ushindi rahisi au ushindani mkali mwaka wa 2027.

Kwa kudumisha hali ya sintofahamu—kumuunga mkono Ruto au ODM kusimamisha mgombeaji—Raila ameonuesha tena asili yake ya kisiasa ya kuwa mgumu kutabirika.

Wafuasi wake walio serikalini sasa wamo njia panda: waendelee kuwa waaminifu kwake ama wazingatie kazi zao chini ya Rais Ruto?

Wachambuzi wa siasa wanasema kauli ya Raila ni, au ni njia ya kujiongezea nafasi ya mazungumzo zaidi na Ruto, au ishara za awali za kutengana.

“Hali si rahisi. Baba ametuweka sehemu ngumu. Tuko serikalini, lakini hatujui kama bado anatuhitaji baada ya 2027,” alisema mbunge wa mrengo wa serikali jumuishi.