Hali tete ya ugatuzi wagonjwa wakiibuka chanzo cha mapato ya kaunti
KAUNTI zipatazo 40 zinategemea ada za hospitali kuendesha shughuli muhimu, hali inayochora picha mbaya ya serikali gatuzi kutegemea watu kuugua, ripoti mpya imefichua.
Ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti (CoB) ya mwaka wa fedha ulioisha Juni 30, 2025 imeonyesha kuwa kaunti hutegemea pakubwa mapato yanayotokana na ada za hospitali, ambazo zinachangia zaidi ya asilimia 50 ya mapato ya ndani (OSR).
Kwa mujibu wa ripoti ya Dkt Margaret Nyakang’o, ni kaunti za Isiolo, Nairobi, Mombasa, Uasin Gishu, Tana River, Samburu na Narok pekee ambazo hazipati mapato makubwa kutoka kwa ada za hospitali – iwe kupitia malipo ya moja kwa moja au madai yaliyolipwa baada ya matibabu.
Dkt Nyakang’o alisema katika kipindi kilichokaguliwa, kaunti zilikusanya Sh67.3 bilioni kama mapato ya ndani, huku zikikosa shabaha ya mapato yaliyokusudiwa kwa Sh20.37 bilioni kwa mwaka huo.
Ripoti hiyo ilionyesha kwamba ukusanyaji wa ada za afya au hospitali ulijumuisha asilimia 37 ya jumla ya mapato ya ndani ya kaunti.
Kwa kaunti kama Bomet, Nyamira, na Homa Bay, mapato ya aina hii yalizidi ya asilimia 70 ya mapato yao ya ndani.
Ripoti ya CoB ilisema hali hii inaweka kaunti katika hatari za kifedha kwa sababu mapato hayo yanapaswa kutumika kwa matumizi ya huduma ndani ya hospitali husika, si matumizi ya jumla ya serikali za kaunti.
“Kutegemea pakubwa hazina ya uboreshaji wa vituo, ambayo inachangia zaidi ya asilimia 50 ya mapato ya ndani kwa kaunti nyingi, kunahatarisha uthabiti wa kifedha. Serikali za kaunti zinapaswa kuunda mikakati halisi ya kuongeza mapato yao na kupunguza kutegemea hazina hiyo,” alisema Dkt Nyakang’o.
Kaunti ya Nyamira ilikuwa na zaidi ya asilimia 81 ya mapato yake yote kutokana na ada za hospitali, ambapo ilikusanya Sh606.6 milioni huku Sh134.53 milioni zikitoka kwa vyanzo vingine vya mapato ya ndani.
Kaunti ya Garissa chini ya Gavana Nathif Jama ilipata zaidi ya asilimia 80 ya Sh478.87 milioni ya mapato yake kutokana na ada za hospitali.
Homa Bay ilikusanya Sh390.67 milioni kutoka kwa vyanzo vingine vya mapato ya ndani huku Sh1.1 bilioni zikitokana na ada za hospitali, sawia na asilimia 74 ya mapato yote ya Sh1.49 bilioni.
Serikali ya kaunti hii ilikuwa na lengo la kukusanya Sh981.07 milioni kutokana na chanzo hiki lakini ilipokea Sh1.02 bilioni kama michango kutoka kwa SHA huku mingine ikiwa malipo ya moja kwa moja.
Zaidi ya asilimia 70 ya mapato ya Kaunti ya Kitui ya Sh895.42 milioni yalitokana na ada za hospitali huku Sh264.1 milioni zikitoka kwa vyanzo vingine.
Kati ya Sh1.44 bilioni za Kakamega, zaidi ya asilimia 62 ya mapato yalitokana na ada za hospitali za Sh894.80 milioni huku Sh448.90 milioni pekee zikitolewa na SHA.
Kericho, zaidi ya nusu ya mapato yake yalitokana na ada za hospitali ya Sh682 milioni huku Sh396 milioni zikitokana na vyanzo vingine.
Sh170.9 milioni pekee zilitoka kwa SHA. Zaidi ya nusu ya mapato ya Kaunti ya Kirinyaga yalitokana na ada za hospitali, ambapo ilikusanya Sh431.5 milioni kutoka jumla ya mapato ya ndani ya Sh852.34 milioni.
Hali kama hiyo pia ilionekana katika Kaunti ya Kisumu ambapo mapato ya jumla ya Sh2.46 bilioni yalijumuisha Sh1.66 bilioni kutokana na ada za hospitali huku Sh803.36 milioni zikitoka vyanzo vingine.
Laikipia pia ilikusanya Sh1.27 bilioni kwa mapato ya ndani lakini zaidi ya nusu zilikuwa ada za hospitali, Sh695.97 milioni, huku Sh70.94 milioni zikitoka SHIF kwa madai yaliyothibitishwa.
Kaunti ya Lamu pia ilikuwa na tatizo kama hilo ambapo mapato yake ya jumla ya Sh233.7 milioni yalichangiwa na Sh139.1 milioni kutoka ada za hospitali huku vyanzo vingine vikirekodi Sh94.6 milioni tu.
Kaunti ya Kisii chini ya Gavana Simba Arati iliripoti mapato ya jumla ya Sh1.59 bilioni lakini zaidi ya asilimia 61 zilitokana na ada za hospitali zilizokuwa Sh982.09 milioni.
Kaunti ilikuwa imepanga kukusanya hadi Sh1.56 bilioni kutoka kwa wagonjwa katika kipindi kilichokaguliwa.
Kwa kaunti ya Nyandarua, jumla ya mapato ya Sh653.24 milioni yalijumuisha Sh282.53 milioni kutoka ada za hospitali huku karibu nusu ya Sh1.45 bilioni za Nyeri zikitokana na mapato ya ada za hospitali.
Mapato ya kaunti ya Siaya ya Sh436 milioni yalijumuisha Sh199 milioni kutoka ada za hospitali.
Kaunti ya Machakos pia ilikusanya Sh755.68 milioni kutoka ada za hospitali kuongeza jumla ya mapato ya Sh2.18 bilioni. Kutoka ada hizo, Sh235.12 milioni pekee zilikuwa michango kutoka SHIF.