Habari za Kitaifa

Hamtatoboa huko Seneti, Nyaribo aambia madiwani waliomuondoa mamlakani

Na RUTH MBULA December 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Nyamira aliyeondolewa mamlakani, Amos Nyaribo, ametaja kung’olewa kwake kuwa batili kwa sababu upigaji kura katika Bunge la Kaunti uligubikwa na udanganyifu.

Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu aondolewe, Bw Nyaribo alisisitiza kuwa mchakato huo tata haukuwa halali, kwani baadhi ya madiwani waliodaiwa kupiga kura dhidi yake sasa wamekana kushiriki zoezi hilo.

“Kulikuwa na udanganyifu. Kwenye bunge kulikuwa na madiwani 19; baadhi hakushiriki, akiwemo mmoja aliye Amerika,” alisema Bw Nyaribo.

Alisema bunge la kaunti lililodai kumng’oa halikutimiza vigezo vinavyohitajika.

“Kwa hivyo wale madiwani wanne wanaodaiwa kupiga kura kwa niaba ya wengine tayari wamewasilisha viapo kukana kushiriki kwao. Ni kweli hakuna ushahidi wowote ambao bunge limepatia mawakili wangu kuthibitisha waliruhusu wawakilishwe.”

Akaongeza, “Hata hawajawasilisha kwa Seneti barua zinazodaiwa kuwaruhusu hao wanne kupiga kura. Huo ni udanganyifu tofauti ambao DCI itashughulikia.”

Alifafanua kuwa mchakato wa kumwondoa gavana lazima uzingatie masharti ya kikatiba yaliyowekwa.

“Kwa upande wa Nyamira, kigezo ni madiwani 24. Hata kwa udanganyifu, hawakufikia idadi hiyo. Tunawaachia Seneti, ambayo ni chombo cha haki,” alisema.

Bw Nyaribo alisema suala hilo “ni rahisi kama ABCD” na akatabiri kuwa litazimwa katika Seneti.

Ameunda timu ya mawakili watano na wasaidizi wa kisheria wawili kumwakilisha Seneti.

Taifa Leo iliona barua kutoka kwa Mutuma Gichuru kwa Spika wa Seneti, Amason Kingi, ikionyesha kuwa atamwakilisha gavana wakati wa kikao cha Seneti.

Barua hiyo ya Novemba 27, 2025 ilisema kwa sehemu: “Gavana wa Kaunti ya Nyamira, Amos Kimwomi Nyaribo, atahudhuria binafsi kikao cha Seneti mnamo Desemba 3 na 4, 2025, na pia atawakilishwa.”

Bw Nyaribo alitaja kuondolewa kwake kama mchakato usio na maana, unaochochewa na siasa za urithi.

“Ni siasa za urithi. Waliharakisha kwa sababu walijua ningepata madiwani zaidi baada ya uchaguzi mdogo wa wadi tatu, jambo ambalo lingefanya isiwezekane kumng’oa gavana. Hakuna pesa zilizopotea; hakuna katiba iliyokiukwa. Bila hayo mawili, hakuna sababu ya kumuondoa gavana.”

Aliwataka wakazi wa Nyamira kuwaadhibu kisiasa madiwani waliopanga kumuondoa katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Kosa kubwa lilikuwa kutambua Bunge Mashinani. Lakini kila nilichofanya kilikuwa kwa maagizo ya mahakama. Sikuhutubia Bunge Mashinani bali Bunge la Kaunti ya Nyamira kwa mwongozo wa mahakama,” alisema.